Mahitaji ya waathirika wa vimbunga Msumbiji bado ni mengi-IOM

Waathirika wa kimbunga Idai na Kenneth nchini Msumbiji, Hap ni Beira mvulana akitizama kupitia dirisha ya darasa lake.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Waathirika wa kimbunga Idai na Kenneth nchini Msumbiji, Hap ni Beira mvulana akitizama kupitia dirisha ya darasa lake.

Mahitaji ya waathirika wa vimbunga Msumbiji bado ni mengi-IOM

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji duniani, IOM António Vitorino hii leo amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Msumbiji ambako ametathmini na kuunga mkono juhudi za msaada wa kibinadamu kufuatia vimbunga viwili vilivyopiga taifa hilo la kusini mwa Afrika mwezi  Machi na Aprili mwaka huu na kuathiri watu milioni 1.8 bila kusahau vifo vya mamia ya watu.

 

Miezi michache tangu majanga hayo watu laki tano wanaendelea kuishi katika makazi yaliyoharibiwa na zaidi ya watu 77,000 wanaishi katika vituo vya hifadhi.

Bwana Vitorino amesema, “kuna mengi ya kufanya na mahitaji ya dharura yanayohitaji kushughulikiwa na kujenga upay Maisha ya wale walioathirika na kimbunga Idai na Kenneth, hususan kwa upande wa chakula, makazi na mbinu za kujipatia kipato,”

IOM imeelezea dhamira yake kusaidia watu wa Msumbiji na kufanya kazi na mamlaka nchini humo na washika dau wa misaada ya kibinadamu katika kurejelea hali ya kawaida baada ya majanga hayo.

IOM imeshukuru serikali ya Msumbiji kwa ushirikiano wao na kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na dharura ya kimbunga Idai na Kenneth.

Tangu mwezi Machi mwaka huu, IOM imesaidia zaidi ya watu laki mbili na elfu themanini walioathirika na vimbunga.

Katika ziara hiyo ya siku mbili, mkuu huyo wa IOM amekutana na viongozi wa serikali ikiwemo, rais Filipe Nyusi na baadhi ya mawaziri na kuzungumzia kuendeleza ushirikiano kusaidia watu wa Msumbiji.