Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkunga wa jadi mkimbizi aliyejitolea kuokoa maisha ya wajawazito warohingya kambini Cox’s Bazar

Mtoa huduma wa kujitolea katika kituo cha afya cha Cox,s Bazaar katika kambi ya wakimbizi akiwa na mama wa miaka 18 na mwanae, Bangladesh 2019
© UNICEF Patrick Brown
Mtoa huduma wa kujitolea katika kituo cha afya cha Cox,s Bazaar katika kambi ya wakimbizi akiwa na mama wa miaka 18 na mwanae, Bangladesh 2019

Mkunga wa jadi mkimbizi aliyejitolea kuokoa maisha ya wajawazito warohingya kambini Cox’s Bazar

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Bangladesh, mkimbizi mmoja kutoka Myanmar ambaye nyumbani alikuwa mkunga wa jadi, sasa anatumia stadi hiyo kuleta nuru kwa wanawake wajawazito kwenye makazi ya wakimbizi wa kirohingya huko Cox’s Bazar.

Shirika la idadi ya watu duniani UNFPA katika makala yake maalum leo siku ya wahudumu wa kibinadamu linammulika mwanamke huyo aliyepatiwa jina la Bibi ambaye mwendo wake kila wakati wa kasi kama anavyozungumza akipita kwenye nyumba zenye wajawazito.

UNFPA inasema jukumu lake alilojipatia ni kusaidia wajawazito hao kujifungua salama, jukumu ambalo alizoea kufanya huko Myanmar ambako alisaidia kuzalisha zaidi ya watoto 4,000.

Bibi anafanya kazi yake hiyo kwenye makazi ya Cox’ Bazar kusini mwa Bangladesh kwa ushirikiano na UNFPA akitembelea wajawazito kukagua afya za ona kuwaelezea juu ya umuhimu wa kwenda kumuona mkunga.

Kwa mujibu wa UNFPA, Bibi huhakikisha kuwa kila anapolala pembeni mwa kitanda chake kuna baibui yake ili aweze kuvaa haraka pindi anapotakiwa kuamka kwenda kumsaidia mjamzito.

UNFPA inasimulia kisa cha karibuni zaidi ambapo usiku wa manane kulikuwa na mfulilizo wa hodi mlangoni kwake ambapo mtoto wa kike wa mjamzito mmoja aitwaye Fatima aliyembelea hivi karibuni alikuwa amekuja kumuarifu kuwa mama yake anahitaji msaada.

“Bibi alipowasili nyumbani kwa Fatima alimkuta amelala chini kwenye mkeka akilia kwa uchungu, na ilibidi kusaka msaada kutoka kituo cha afya kinachopatiwa usaidizi na UNFPA lakini tatizo hawakuwa na usafiri,” imesema makala hiyo ya UNFPA.

 

Giza totoro ni changamoto kubwa Cox’ Bazar

Ndani ya kambi hiyo kubwa zaidi duniani, takribani kila mtu analala saa mbili usiku kwa sababu hakuna umeme na maeneo yenye taa zinazotumia nishati ya sola ni machache sana kwa hiyo kwa mjamzito kupata uchungu nyakati za usiku ni tatizo kubwa.

“Inakuwa ni changamoto zaidi kwa warohingya nyakati za usiku kufikia vituo vinavyotoa huduma za uzazi,” anasema Anne Marie Brennan ambaye ni mtaalamu wa UNFPA anayehusika na masuala ya ukunga akisema kuwa  “si tu kwamba hakuna mwanga wa kutosha, bali maeneo mengine hayafikiki kwa gari, na pia inakuwa vigumu kwa simu kupata mtandao.”

 Bibi na mtoto yule wa kike walitoka pamoja gizani kwenye kambi hiyo ambayo nyakati za usiku hakuna mtu kabisa kwani wote wamelala, hivyo walitembea taratibu wakisaka teksi ya kienyeji ambayo ni bajaji.

Walitembea kwa nusu saa wakishikana mikono bila kuona mtu yeyote zaidi ya mbwa wanaoranda randa mitaani, na bado  hawakuweza kupata usafiri.

Hata hivyo kadri kulipokuwa kunakaribia kukucha, waliona bajaji na kuisimamisha, na katika kambi hii madereva wa bajaji wanafahamu kuwa wanalipwa iwapo watamfikisha salama mjamzito kwenye kituo cha afya kinachopatiwa msaada na UNFPA.

Hatimaye Fatima alifikishwa kliniki na kujifungua salama nusu saa tu baada ya kuwasili.