Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye Sudan nuru yaingia, UN yapongeza

Waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum

Hatimaye Sudan nuru yaingia, UN yapongeza

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amewapongeza kwa moyo mkunjufu wananchi wa Sudan kwa hatua muhimu ya leo ya kutia saini nyaraka za kuelekea mpito wa serikali ya kiraia.

Hatua hii inakuja baada ya miezi kidhaa ya mvutano na ghasia kati ya raia na mamlaka za jeshi zilizochukua madaraka kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Omar al Bashir mwezi Aprili mwaka huu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa  Stéphane Dujarric, kupitia taarifa aliyotoa leo mjini New York, Marekani amemnukuu Katibu Mkuu akipongeza pia dhima ya Muungano wa Afrika, AU na Ethiopia katika kusimamia na kuratibu mazungumzo yaliyoongozwa na wasudan wenyewe.

“Katibu Mkuu anasubiria kwa hamu kushirikiana na kusaidia taasisi tawala za mpito. Amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia mchakato wa mpito na kusaka matarajio ya muda mrefu ya wananchi wa Sudan juu ya demokrasia na amani,” imesema taarifa hiyo.

Katibu Mkuu pia amesisitiza umuhimu wa kufungua njia kwa ajili ya kuikwamua Sudan kiuchumi na kijamii na kuiweka nchi hiyo kwenye mwelekeo wa maendeleo endelevu kwa maslahi ya wananchi wote.

“Umoja wa Mataifa uko tayari kushirikiana na wadau wa kimataifa na kusaidia Sudan katika mwelekeo huo,” imetamatisha taarifa hiyo.

Waandamanaji wakiandaman nje ya makao makuu ya vikosi vilivyojihami vya Sudan katika mji mkuu, Khartoum.
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji wakiandaman nje ya makao makuu ya vikosi vilivyojihami vya Sudan katika mji mkuu, Khartoum.

Makubaliano yenyewe

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa makubaliano hayo yametiwa saini mjini Khartoum baina ya Mohammed ‘Hemeti’ Dogolo, mtu anayeonekana kuwa na ushawishi mkubwa Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan kwa niaba ya Baraza la kijeshi na Ahmed al-Rabie wa Alliance for Freedom and Change, ambalo ni shirikisho la waandamanaji waliokuwa wanadai demokrasia.

Makubaliano sasa yanafungua njia ya kuwa na Baraza jipya ya usimamizi likijumuisha raia na wanajeshi na hivyo kuelekea katika uchaguzi wa serikali ya kiraia.

Halikadhalika Baraza hilo la usimamizi litakuwa na raia 6, majenerali 5 na litaendesha Sudan hadi wakati wa uchaguzi.

Pande hizo zimekubaliana kuwa na mzunguko wa uenyekiti wa Baraza hilo kwa miaka mitatu na Waziri Mkuu wa kuchaguliwa na raia atachaguliwa wiki ijayo.