Mkurugenzi mkuu wa UNESCO aisihi Mexico iangazie mauaji ya wanahabari watatu.

16 Agosti 2019

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay amelalamikia mauaji ya wanahabari watatu nchini Mexico, ambao ni Edgar Alberto Nava López, Rogelio Barragán Pérez, na Jorge Ruiz Vázquez, akitoa wito kwa mamlaka kuchunguza matendo hayo yaliyofanywa kati ya mwishoni mwa mwezi Julai na tarehe 2 Agosti.

Taarifa ya UNESCO iliyotolewa leo huko Paris, Ufaransa imesema wanahabari wote watatu awali walikuwa wameripoti kuhusu kutishiwa maisha yao kutokana na kazi yao.

“Ninalaani mauaji ya Jorge Ruiz Vázquez, Edgar Alberto Nava López, na Rogelio Barragán Pérez,” amesema amesema Bi Azoulay na kuongeza, “ninatoa wito kwa mamlaka kuchunguza mauaji haya na kuwaleta katika mikono ya sheria walioyatekeleza. Pia ninazisihi mamlaka kuchukua hatua za kuwalinda wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa kuwa wanafanya jukumu muhimu la kuilinda demokrasia na utawala wa sheria.”

Rogelio Barragán Pérez Mkurugenzi wa tovuti ya Guerrero Al Instante alikutwa amefariki katika buti ya gari mnano tarehe 30 Julai huko Zacatepac Katila jimbo la Morelos.

Naye Edgar Alberto Nava López, mwanzilishi wa tovuti ya habari ya La Verdad de Zihuatanejo alipigwa risasi na kufa Agosti pili katika jimbo la Guerrero na iliripotiwa kuwa alikuwa amepokea vitisho kutokana na kuripoti uhalifu.

Jorge Ruiz Vázquez, ripota wa Grafico de Xalapa alipigwa risasi na kufa katika makazi yake huko Actopan jimbo la Veracruz siku aliyouawa Edgar Alberto Nava López yaani Agosti pili. Awali alikuwa ameripoti kuhusu kupokea vitisho vinavyohusishwa na kazi yake ya kuripoti vitendo vya rushwa. Ruiz Vázquez aliuawa siku chache kabla ya tarehe iliyopangwa kwa yeye kutoa ushahidi kwa mamlaka juu ya vitisho dhidi yake.

UNESCO inahimiza na kukuza usalama wa wanahabari kupitia ukuzaji uelewa kote duniani, kuwajengea uwezo latika masuala mbalimbali hasa katika mfumo wa utendaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa wanahabari.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud