Matangazo, uchagizaji na ufadhili wa tumbaku lazima ukomeshwe:WHO

15 Agosti 2019

Shirika la afya ulimwenguni WHO leo limerejea wito wake wa mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa bidhaa za tumbaku, FCTC ,kwa kuzitaka serikali utekeleza hatua za kupiga marufuku matangazo, uchagizaji na ufadhili wa bidhaa za tumbaku katika matamasha na mikutano ya kimataifa ili matukio hayo yanakuwa huru bila tumbaku na washiriki wake hawafadhiliwi  na makampuni ya bidhaa za tumbaku.

Wito huo wa WHO umesisitiza kwamba dunia ni lazima ishikamane kukomesha mkakati wa sekta ya tumbaku wa kuuza bidhaa zake ambazo husababisha uraibu, maradhi na vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka.

Wito huu umekuja tena kufufuatia taarifa kwamba makampuni ya tumbaku yanadhamiria kuanzisha ushirika mpya na serikali ili kufadhili matukio, mikutano au matamasha ya kimataifa katika nchi ambayo tayari iliridhia mkataba wa Who wa kudhibiti tumbaku (FCTC)

Kwa mujibu wa WHO kampuni ya kimataifa ya Philip Morris (PMI) hivi karibuni imetangaza ushirika na serikali ya Uswisi ili kufadhili  banda la nchi hiyo mjini Dubai nchini Falme za Kiarabu, wakati wa tamasha la kimataifa la Expo 2020.

Hata hivyo serikali ya Uswisi imeamua kutokubali ufadhili huo hatua ambayo imekaribishwa na WHO na kuchukua fursa hiyo kuikumbusha serikali ya Uswisi kuridhia mkataba wa FCTC kwani nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa ambayo bado hayajafanya hivyo.

Moja ya vipengee vya mkataba huo vinataka serikali kuchukua hatua za kulinda afya ya umma kwa sera mbalimbali za kudhibiti matakwa ya makambuni ya bidhaa za tumbaku.

WHO inasema kutangaza makampuni ambayo yanaongoza duniani kwa uzalishaji wa bidhaa za tumbaku na sigara , bidhaa pekee zinazofahamika kukatili Maisha ya nusu ya watumiaji wake ni kinyume na kaulimbiu ya maonyesho hayo ya Dubai ya Expo 2020 ambayo ni “kuunganisha fikra, kuunda mustakbali bora”.

Hivyo imesema serikali ni lazima zichukue hatua za kupunguza idadi ya watu wanaoanza au kuendelea kuvuta sigara, kuchagiza afya na kulinda vizazi vijavyo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud