Mustakabali wa elimu kwa watoto na barubaru wa kirohingya uko hatarini- UNICEF

16 Agosti 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema miaka miwili ya harakati za kila uchao za kujikwamua kimaisha kwa warohingya waliosaka hifadhi nchini Bangladesh zimetumbukiza nyongo mustakabali wa elimu kwa kizazi kizima

Watoto wa wakimbizi warohingya wakishiriki kwenye mtaalamu wa vijana au GEMS katika moja ya maeneo rafiki kwa wanawake huko kambini Cox's Bazar nchini Bangladesh
UNFPA Bangladesh/Allison Joyce
Watoto wa wakimbizi warohingya wakishiriki kwenye mtaalamu wa vijana au GEMS katika moja ya maeneo rafiki kwa wanawake huko kambini Cox's Bazar nchini Bangladesh

Miaka miwili imetimu tangu waislamu 745,000 wa kabila la rohingya wakimbie nchi yao ya Myanmar kutokana na mateso na mauaji na hii leo UNICEF imetoa kauli kwenye ripoti inayomulika zaidi watoto na vijana.

Katika ripoti hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema suala la kuweza kuishi tu siku kwa siku si jambo toshelezi kwa watoto na vijana wa kirohingya wanaoishi kwenye kambi Bangladesh.

Badala yake amesema ni muhimu makundi hayo yakapatiwa mafunzo na stadi bora za kujiendeleza kwa ajili ya mustakabali wao.

Bi. Fore amesema bila fursa za kutosha za kujifunza, vijana wanatumbukia kwenye mtego wa wauza madawa ya kulevya na wasafirishaji haramu ambao wanawaeleza kuwa watawatorosha kutoka Bangladesh.

Elimu inaweza kuepusha hatari kama vile usafirishwaji haramu na ndoa za mapema

Ripoti hiyo inasema kuwa wanawake na wasichana wanakabiliwa na ukatili na manyanyaso hususan usiku, ikiongeza kuwa, “kuwapatia watoto elimu na stadi wanazohitaji ni jawabu la kuwaepusha na matukio hayo hatari.”

Kando mwa kambi ya Kutupalong ambayo ni kamazi ya warohingya 630,000, mamia ya maelfu ya wengine wao wamesaka hifadhi kwenye eneo la Cox’s Bazar karibu na mpaka na Myanmar.

UNICEF inasema kuwa mazingira katika maeneo hayo mara nyingine yanaelezwa nwa wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kuwa si mazuri, na ndio maana kila wakati wadau hao wanatoa maonyo ya madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya za hewa zitokanazo na pepo za monsuni na mafuriko kwa kuzingatia kuwa makazi yao ni kwenye mahema.

Ripoti ya UNICEF inasema kuwa kati ya tarehe 21 mwezi Aprili mwaka hu una tarehe 18 mwezi uliopita wa Julai, mamlaka kwenye kambi hiyo walisajili vifo 10 na majeruhi 42 kutokana na pepo za monsuni. Miongoni mwa waliokufa ni watoto 6.

Kutokana na mazingira kutokuwa tayari kwa warohingya kurejea nyumbani Myanmar, ripoti imenukuu shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR likisema kuwa huduma za msingi za umma zimepelekwa huko Cox’s Bazar.

Huduma hizo ni pamoja na zile za afya, lishe, maji, huduma za kujisafi ambapo serikali ya Bangladesh inaongoza harakati hizo.

Elimu yasalia ndoto kwa watoto na vijana warohingya

 Ripoti hiyo ya UNICEF inasisitiza kuwa wakati janga la wakimbizi likiendelea, watoto na vijana wakihaha kupitisha siku ili waweze kuishi, mustakabali wa elimu uko mashakani.

UNICEF inasema watoto 280,000 wenye umri wa kati ya miaka  4 hadi hivi sasa wanapata msaada wa elimu. “Kati  yao hao, 192,000 wako katika vituo vya mafunzo, lakini zaidi ya 25,000 hawahudhurii mafunzo hayo.”

Wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 18 wanakosa elimu

UNICEF inasema kinachotia mashaka zaidi ni kwamba takribani watoto wenye umri wa kuanzi amiaka 15 hadi 18 hawapati fursa yoyote ya elimu ikimulika mtoto mmoja Abdullah mwenye umri wa miaka 18 anayeishi makazi ya Kutupalong.

Abdullah anasema alisoma masomo sita huko Myanmar, “lakini nilipofika hapa hakukuwepo na njia yoyote ya kuendelea. Nadhani tusipopata elimu hapa kambini, hali yetu itakuwa mbaya.”

Ikitoa ombi lake kwa serikali za Bangladesh na Myanmar, UNICEF na mashirika mengine yametoa wito kwa matumizi ya rasilimali za kitaifa, kama vile mitaala, miongozi ya mafunzo na mbinu za tathmini ili kusaidia kuwapatia watoto wa kirohingya mfumo bora zaidi wa elmu.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF amesema “kuwapatia vifaa vya kujifunza ni kazi kubwa sana na inaweza kufanikiwa kama tutaungwa mkono na wadau wote lakini matumaini ya kizazi cha watoto na barubaru yako hatarini na hatupaswi kuwaangusha.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter