Mwanamke fundi stadi wa magari  kutoka Kenya atoa changamoto kwa wasichana na wanawake kufanya kazi za “wanaume”

15 Agosti 2019

Kwa muda mrefu kuna baadhi ya kazi ambazo kwa kawaida zilizoeleka kuwa ni kazi za jinsia moja na wala sio nyingine lakini Christina Wambulu  mwanamke mwenye umri wa miaka 40 kutoka nchini Kenya amekata kauli kwamba kitu muhimu katika utekelezaji wa kazi yoyote ni stadi na maarifa wala sio jinsia.

Video ya Umoja wa Mataifa kuhusu maswala ya jinsia nchini Kenya inamyonesha Bi Christina akiwa anavaa vazi lake la njano ambalo ni sare ya kawaida kwa fundi stadi wa magari , akiwa mjini Kakuma Kaskazini mwa Kenya. Mwanamke huyu ambaye ni mama wa watoto watatu na mwenye uzoefu wa miaka ishirini anasema, "wakati nimeanza kufanya kazi hii sio kwa ajili ya mafunzo niiyoyapata lakini ni kutokana na kipaji changu na hii kazi inaniwezesha kukidhi mahitaji yangu na ya watoto wangu kwa sababu mimi ni mjane."

Bi. Wambulu anasisitiza kwamba mwanamke anaweza kufanya kazi nzuri kuliko hata mwanamume na hivyo kubobea katika kazi hiyo, "kazi yangu ni nzuri na ndio maana watu wanapenda kazi yangu, niko wazi katika utekelezaji wa kazi yangu, mara kwa mara watu hushangaa au kusema kuwa mimi ni mchafu lakini hiyo ndio raha yangu, kwani uchafu huo unanipatia kipato."

Bi Wambulu akiwa anakarabati gari katika karakana ya kukarabati magari anatoa changamoto kwa wanawake na wasichana kufanya kazi ambazo hazikuzoeleka kufanywa na wanawake akisema, "wanawake na wasichana wanaweza kufanya kazi hii, na hawapaswi kuona kama ni kazi ngumu cha msingi ni kuifanya. Nawasihi wajaribu kazi hii kwani si ngumu."

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud