Kuokoa maisha ya watoto waliokwama Mediterranea kupewe kipaumbele badala ya siasa-UNICEF

15 Agosti 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema linasikitishwa kwamba kwa mara nyingine siasa zimepewa kipaumbele badala ya kuokoa maisha ya watoto ambao wamekwama kwenye bahari ya Mediterranea. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa UNICEF Ulaya na Asia ya kati na mratibu wa maswala ya wakimbizi na wahamiaji Ulaya, Bi Afshan Khan “watoto takriban 130 wako kwenye meli. Yaelezwa kuwa ni watoto 11 tu kati ya watoto 103 walioko ndani ya meli ya Viking Ocean wameandamana na mzazi au mlezi.

Taarifa ya UNICEF imesema wengi wa watoto hao, ambao wanakimbia umaskini, mizozo na mateso yasiofikirika wana haki ya kuwa salama na kulindwa.

UNICEF imetoa wito kuwa kutoka salama kwenye bandari kufanikishwe ili watoto wote pamoja na wale walioko kwenye meli hizo mbili wakatoka salama.

Bi.Khan kupitia taarifa hiyo amesema, “kupoteza maisha kwa watu Mediterranea ya kati msimu huu wa joto kali kunaashiria haja ya haraka ya kuimarisha juhudi za kutafuta na kuokoa maisha. Kuokoa watoto walio hatarini, wanawake na wanaume haipaswi kuwa hatia.”

UNICEF imeongeza kwamba maeneo ya kuwapokea na kuwagundua wakimbizi na wahamiaji watoto yanapaswa kuwa salama na toshelezi pamoja na ufikiaji wa huduma ya afya, msaada wa kisaikolojia na kijamii na utaratibu wa kuomba hifadhi. Aidha mwitikio ambao unatoa kipaumbele kuhifadhi watoto na kuharakisha kuunganisha familia kutoka kwa matifa ya muungano wa Ulaya unahitajika.

UNICEF imekaribisha hatua za hivi karibuni kuelekea mpango wa kuimarisha umoja na majukumu miongoni mwa serikali za Ulaya.

Ikihitimisha taarifa hiyo ya UNICEF imesema, “watoto hawapaswi kukwama baharini au kuzama kwenye fukwe za Ulaya. Majadiliano ya kisiasa yanapaswa kubadilika na kuwa hatua za kanda nzima ambazo zitaokoa maisha na kumaliza mateso zaidi.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud