Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu mpya wa UNAIDS ni Winnie Byanyima kutoka Uganda

Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwenye Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Amanda Voisard
Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwenye Umoja wa Mataifa.

Mkuu mpya wa UNAIDS ni Winnie Byanyima kutoka Uganda

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amemteua  Winifred ‘Winnie’ Karagwa Byanyima wa Uganda kuwa ndiye mkurugenzi mtendaji mpya wa shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi, UNAIDS.

Uteuzi huo umefuatia utafiti na mchakato wa muda mrefu ulioongozwa na mashirika wadhamini chini ya uwenyekiti wa Dkt Natalia Kanem, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA, mchakato ambao ulijumuisha mahojiano na majadiliano na pande zote husika kupitia bodi ya uratibu wa program za UNAIDS.

Bi. Byanyima  anachukua nafasi ya Michel Sidibé ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa afya na ustawi wa jamii wa Mali.  Katibu Mkuu amemshukuru Dkt. Sidibé kwa kuliongoza shirika la UNAIDS tangu mwaka 2009 hadi 2019 akiwa msitari wa mbele katika kukabilina na changamoto za kimataifa za HIV na ukimwi.

Bi. Byanyima atakuja na uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya uwezo wa serikali, mashirika mbalimbali, sekta binafsi na asasi za kiiraia katika kutokomeza virusi vya HIV na ukimwi kwa jamii zote duniani.

Bi. Byanyima amekuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataifa la Oxifam tangu mwaka 20013. Kabla ya hapo kwa miaka saba alikuwa mkurugenzi wa idara ya jinsia na maendeleo katika shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP.

Alianza safari yake kama mwanaharakati wa kupigania jamii zilizotengwa na wanawake miaka 30 iliyopita alipokuwa mbunge katika bunge la kitaifa nchini Uganda.

Na mwaka 2004, alitangazwa kuwa mkurugenzi wa wanawake na maendeleo katika tume ya muungano wa Afrika (AU) akifanya kazi katika masuala ya mikataba na haki za wanawake barani afrika chombo cha kimataifa cha haki za binadamu ambacho baadaye kilikuwa nyenzo muhimu katika kuelekea kupunguza athari za maambukizi ya HIV katika Maisha ya wanawake wengi barani Afrika.

Bi. Byanyima ana shahada ya uzamili katika masuala ya uhandisi wa mitambo  ikijikita katika uhifadhi wa nishati na mazingira kutoka kutoka kwenye taasisi ya teknolojia ya Cranfield  Uingereza na pia ana shada ya kwanza masuala ya uhandisi wa masuala ya ndege kutoka chuko kikuu cha Manchester nchini Uingereza.   Anazungumza Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa kidogo. Ameolewa na ana mtoto mmoja wa kiume.

Katibu Mkuu amemshukuru naibu mkurugenzi mtendaji wa idara ya utawala ya UNAIDS Gunilla Carlsson kutoka Sweden, kwa huduma yake aliyoitoa kama kaiimu Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo.