Ukimbizi waweza kuwa baraka kwako na kwa wengine:Mkimbizi Jenipher 

15 Agosti 2019

Hali ya kuwa mkimbizi kwa sababu yoyote ile ni changamoto kubwa hasa kwa kutojua mustakabali wako na endapo ulikoikimbia kutatengamaa. Mkimbizi Jenipher Mutamba toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambaye sasa anaishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Oruchinga nchini Uganda anasema wakati mwingine ukimbizi hufungua mlango wa baraka katika maisha. John Kibego na taarifa zaidi

 Jenipher na familia yake waliwasili Uganda miaka saba iliyopita wakikimbia vita nchini DRC, anakumbuka hali ilivyokuwa mbaya hata akalazimika kufungasha virago akisema kuwa, “tulikuwa kanisani tukasikia milio ya risasi, sasa wakati tunatoka tukatuta watu kutoka kijijini kwentu wanakimbia, nasi tukatoka kanisani tukaungana nao kukimbia, hatukufika nyumbani , mi nilikuwa nawaza tuu sijui tutakufa au tutapona, watu walikuwa wengi.”

Hatimaye waliwasili Uganda na kupata hifadhi katika makazi ya wakimbizi ya Oruchinga. Mwanzo ulikuwa mgumu hasa kuhudumia familia yake. Na kama walivyo wanawake wengi wakimbizi alikwenda mbali kusaka mahitaji kama kuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani au kuuza na na huko walikutana na changamoto nyingi ikiwemo ukatili wa kingono. Katika hali hiyo Jenipher anasema, "tulikuwa tunakutana na wanaumme mahali ambako wanachoma mkaa wanakuambia tutakupa mkaa bure, sasa unaona huwezi kurudi nyumbani bila kitu na huna hela unalazimika”

Jenipher akaona ni lazima apate jawabu la mtihani huo. Kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na wadau wengine akaanzisha kikundi cha wanawake wakimbizi cha kuweka na kukopa ambacho kimebadili maisha yao, kwani kikundi kinawasaidia kuhudumia familia zao na pia kuchangia uchumi wa jamii zao na kwamba“tunawapa wanawwake kwanza fedha kidogo zinazotosheleza kuanzisha biashara ili tuwafundishe , na tukiona wameshajua biashara tunamuongeza pesa. Ndio maana unaona watoto katika makazi ya Oruchinga wanaweza kwenda shule, lakini hapo awali walikuwa wanazungunga tu.”

Jenipher pia amepata njia nyingine ya kusaidia jamii kwa kujitolea kufanya kazi na timu ya serikali, UNHCR na washirika wengine kuhakiki wakimbizi kwa kutumia teknolojia ya kisasa akisema “tatizo kubwa la wakimbizi ni mtu kukimbia na kutokuwa na msimamo, sasa tunaka kujaribisha kama UNHCR itatusaidia ili kuwe na mashine kama hizi dunia nzima ili kama ni mkimbizi Uganda ajue kama maisha yake yako Uganda”

Jenipher ameleta matumaini na kufanya maisha kuwa bora kwa wakimbizi wenzie.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter