Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UN-Habitat wa kupima ramani ya ardhi ni habari njema kwa wakazi vijijini Uganda

Kuwepo kwa amani kunawezesha wakulima kama huyo pichani anayelima mihogo kuweza kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa chakula.
FAO/Giulio Napolitano
Kuwepo kwa amani kunawezesha wakulima kama huyo pichani anayelima mihogo kuweza kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa chakula.

Mradi wa UN-Habitat wa kupima ramani ya ardhi ni habari njema kwa wakazi vijijini Uganda

Amani na Usalama

Uganda ni moja ya nchi zilizo na idadi kubwa ya watu na idadi hiyo inaongezeka kila uchao. Kwa sasa nchi hiyo ina takriban watu milioni 40 na zaidi ya asilimia 75 wanaishi vijijini na asilimia 80 ya watu hao wako katika mashamba ya kurithi ambayo mengi hazijaandikishwa, kupimwa  wala kuingizwa katika ramani.

Hii ni sauti ya Paulino Leru, mkulima kutoka wilaya ya Adjumani kaskazini mwa Uganda, anasema ameishi katika ardhi yake tangu mwaka 1973 kwa takriban miaka 36. Mkulima Leru ni mfano tu wa hali ya wakulima wengi ambao licha ya kuishi katika ardhi walizorithi kwa miaka mingi hawana stakabadhi zozote za umiliki wake.

Ni kwa kuzingatia hilo ndipo Shrika la makazi la Umoja wa Mataifa UN-Habitat na muungano wa kimataifa wa mbinu za ardhi GLTN kwa ushirikiano na serikali ya Uganda na wadau wengine waliungana kutekeleza mradi wa kuimarisha umiliki wa ardhi salama kwa ajili ya kaya vijijini hususan wanawake, vijana na makundi ya watu walio hatarini katika baadhi ya maeneo nchini humo. Adjumani ni moja ya maeneo matatu yaliyochaguliwa na mkulima Leru ni miongoni mwa wanufaika wa mradi.

Mkulima Leru anasema, “Nina furaha sana kupata hati hiyo kesho kwa sababu ni hakikisho kwamba hata nikifa watoto wangu watakuwa na haki ya kumilika shamba ambalo limeandikishwa kwa jina langu.”

Moja ya vikwazo vya kupima ramani ya ardhi ni gharama ambapo Christine Mususi wa kitengo cha mahusiano ya nje kwenye UN-Habitat amesema“gharama ya kupima ramani ya ardhi na kusimamia imepunguzwa kutoka dola mia sita hadi dola ishirini ambayo ni sawa na gharama ya kuku wawili, hii ikimanisha kwamba mmiliki yeyote wa ardhi anaweza kugharamia hiyo.”

Mradi pia umeweka mbinu za kuhifadhi rekodi za kidijitali kwa ajili ya siku za baadaye. Kwa wenyeji wanaopokea hati za kumiliki ardhi ni furaha tele.Marietta Pido ni mmoja wao akisema kuwa, “Ninaimani kwamba ardhi yangu imepimwa vilivyo na wajukuu zangu hawataondolewa pale na mtu yeyote.”