Dawa mbili zilizoko kwenye majaribio zimeonesha uwezekano mkubwa kutibu Ebola-WHO

14 Agosti 2019

Dawa mbili mpya zinazojaribiwa kwa wagonja wa Ebola nchini DRC zimeonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaweza kupona ikiwa watapatiwa matibabu ndani ya siku tatu tangu kuanza kuonesha dalili za ugonjwa huo, limesema shirika la afya Ulimwenguni WHO. 

Jaribio lilianza mwezi Novemba mwaka jana 2018 likilinganisha tiba nne, mbili kati ya hizo yaani REGN-EB3 na mAb114 zimeonesha matoneo mazuri kuliko nyingine.

WHO imethibitisha kuwa matokeo haya yanaridhisha kwa kiasi kikubwa kiasi jopo huru la kufuatilia jaribio limeshauri kufikiwa kwa mapema kwa mwisho wa jaribio hilo la dawa ya Ebola na sasa wagonjwa wote wenye Ebola nchini DRC watatibiwa kwa dawa hizi mbili.

Msemaji wa WHO Christian Lindmeir amewaambia wanahabari mjini Geneva Uswisi,

(Sauti ya Christian Lindmeir)

“maboresho yamefanyika kwa matibabu ya wagonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Wagonjwa sasa watapokea moja ya dawa hizi za tiba ya majaribio ya Ebola. Ni Regeneron au mAb114. Uhakiki wa majaribio haya yaliyoangaliwa na jopo huru umeona kuwa tiba hizi zimefanya vizuri kuliko zile nyingine mbili.

 WHO inasema kiwango cha vifo kwa dawa ya REGN-EB3 na mAb114 ilikuwa asilimia 34, na dawa zilifanya hata vizuri zaidi kwa wagonjwa ambao walipata matibabu mapema ndani ya siku tatu za maambukizi. Kwa mazingira hayo, vifo vilipungua hadi kufikia asilimia 6 kwa dawa ya REGN-EB3 na asilimia 11 kwa dawa ya mAb114.

Bwana Lindmeir anaongeza kwa kusema,

(Sauti ya Christian Lindmeir)

“hii ni habari njema na itaokoa maisha na kutusogeza karibu kupata tiba bora ya Ebola.”

Pamoja na kuwa dawa hizi ni vitu muhimu katika mapambano dhidi ya Ebola, WHO inasema matumizi ya chanjo, na pia dawa hizi mbili zinazoleta matumaini, pekee havitatokomeza Ebola. Hapo Lindmeir anafafanua,

(Sauti ya Christian Lindmeir)

“tiba kamili inaweza isiwezekane hata kama una dawa inayofanya kazi kwa asilimia 100, bado inahitaji kipengele muhimu cha mtu kufika katika eneo la matibabu mapema zaidi.”

WHO inasisitiza kujikinga, kufanya uchunguzi, na pia kuwapokea wanaohusika na mapambano dhidi ya Ebola katika jamii kuwa ni miongoni mwa  masuala muhimu katika mapambano haya. Watu wote wanahamasishwa kuwaangalia wapendwa wao na kutafuta huduma ya afya haraka iwezekanavyo pindi dalili zinapojitokeza.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud