Idadi ya yatima kutokana na Ebola DRC yaongezeka maradufu- UNICEF

13 Agosti 2019

Idadi ya watoto walioachwa yatima au bila walezi kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo , DRC imeongezeka zaidi ya maradufu tangu mwezi Aprili mwaka huu na huduma za haraka zinahitajika katika majimbo yaliyoathirika zaidi ya Ituri na Kivu Kaskazini limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Flora Nducha na taarifa zaidi

Kivu Kaskazini harakati za kupambana na Ebola zikiendelea UNICEF na washirika wake wanasema wameorodhesha watoto 1380 ambao ni yatima  DRC ikimaanisha watoto hao wamepoteza wazazi wao wote ama mmoja kutokana na Ebola tangu mlipuko huo ulipoanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Katika kipindi hichohicho watoto wengine 2,469 wametenganishwa na wazazi wao au walezi, ama kuachwa peke yao kwa sababu watu wazima wanafanyiwa uchunguzi au kupatiwa matibabu, ama wametengwa kwa kuwa walikutana na mtu aliyeathirika na Ebola.

Kwa mujibu wa Pierre Ferry mkuu wa program za ulinzi wa watoto wa UNICEF nchini DRC “ugonjwa huu umekuwa jinamizi kubwa  hususan kwa watoto, watoto washuhudia wazazi wao wakipoteza maisha mbele yao au wakiona ndugu zao wakichukuliwa kupelekwa kwenye vituo vya matibabu vya Ebola bila kujua lini au endapo watarejea. Wameghubikwa na simanzi huku pia wakijaribu kuwafariji wadogo zao. Wengi wao wanakabiliwa na ubaguzi, unyanyapaa na kutengwa."

Merxie Mercado ni msemaji wa UNICEF Geneva anasema UNICEF inashirikiana kwa karibu na wadau na jamii ili kubwabaini haraka watoto walioathirika na kuwapa msaada unaohitajika akisema kuwa, “ongezeko hili la haraka linahitaji  huduma maalum haraka ili kushughulikia kwa kina mahitaji ya kisaikolojia, kimwili na kijamii ya watoto hawa. Hadi leo UNICEF imewapa mafunzo wataalam wa saikolojia na wasaidizi 906 ambao wanaaminiwa na jamii kutoa msaada mbalimbali kwa yatima na watoto waliotenganishwa.”

Ameongeza kuwa ukizingatia idadi iliyoongezeka zaidi ya mara mbili jitihada zaidi zinahitajika haraka kuongeza msaada huo hususani katika eneo la Beni ambalo limeshuhudia ongezeko kubwa la watoto yatima.

UNICEF inasema kwa yatima ambao wamepoteza wazazi wote mahitaji yao ni ya muda mrefu, na wataalam wa saikolojia wanajitahidi kuwawekwa na ndugu wa familia zao japo si jambo rahisi kutokana na changamoto za kiuchumi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud