Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninaweza nisiwe na pesa lakini nina moyo kwa ajili ya wale wanaokuja-Carmen

Watoto hawa ni miongoni mwa mamilioni ya wavenezuela wanaoikimbia nchi yao, hapa wakisubiri katika kituo cha uhamiaji ili kupata vibali vya kusafiri na kuingia Ecuador (2019)
UNICEF/Santiago Arcos
Watoto hawa ni miongoni mwa mamilioni ya wavenezuela wanaoikimbia nchi yao, hapa wakisubiri katika kituo cha uhamiaji ili kupata vibali vya kusafiri na kuingia Ecuador (2019)

Ninaweza nisiwe na pesa lakini nina moyo kwa ajili ya wale wanaokuja-Carmen

Wahamiaji na Wakimbizi

Kutoa ni moyo, walisema wahenga. Nchini Ecuador, mwanamke mmoja mmiliki wa Hosteli ndogo alipowaona wavenezuela wakifika nchini mwake Ecuador, mara moja aliona anapaswa kutoa msaada bila malipo. Ameendelea na huduma hiyo na sasa wengi wamekuwa sehemu ya familia yake.

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, inamwonesha mwanamke huyo anayefahamika kwa jina Carmen, kwa vicheko na bashaha akikumbatiana na wakimbizi na wahamiaji waliofika katika hostel yake mjini El Juncal. Kisha Carmen anaonekana katika pilika za hapa na pale kuweka mambo sawa kwa wageni wake na anasema,

(Sauti ya Carmen)

“Wana machaguo mawili, la kwanza ni kuendelea na safari yao kwenye saa kumi na moja au kumi na mbili za jioni. Lakini chaguo la pili ni kuja katika sehemu ya Bi Carmen au Bi Candela, kama wavenezuela wanavyoniita. Wanaweza kuoga au kupata mlo, au sehemu ya kulala.”

Kila usiku watu 20 hadi 70 hulala katika hosteli ya Bi Carmen kabla ya kuendelea na safari yao.Wengine wanaamua kubaki hapo kwa Bi Carmen. Mmoja wa wageni wa hosteli hiyo ni Daniel kutoka Venezuela anasema,

(Sauti ya Daniel)

“Tulikuwa tumechoka na tumechafuka, tukaja hapa kwa mwanamke huyu na sasa amekuwa kama mama yetu.”

Wageni wapya wanaowasili wamekuwa sehemu ya familia ya Bi Carmen. Bi Carmen mwenyewe anaeleza akiwarejelea wote kama watoto wake,

(Sauti ya Bi Carmen)

 “Watoto wangu wote wanaoona ninachokifanya, wengi wao huja kunisaidia kupakua chakula, hukaa na kuongea, kusikiliza na hata kulia pamoja. Ninafahamu, miongoni mwao kuna atakayekuwa mkarimu. Hilo ndilo jambo pekee la muhimu katika maisha. Ninaweza nikawa sina pesa, lakini nina moyo kwa wale wanaokuja.”