WFP yakaribisha makubaliano ya kuiwezesha kusambaza tena chakula Sana’a

9 Agosti 2019

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limekaribisha hatua chanya na muhimu zilizochukuliwa na wahouthi wanaodhibiti mji mkuu wa Yemen, Sana’a, hatua ambazo zinalenga kuhakika misaada ya kibinadamu inafikia wahitaji zaidi ambao ni watoto, wanawake na wanaume kwenye maeneo yanayodhibtiwa na mamlaka hizo.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Roma, Italia imesema kuwa nyaraka iliyotiwa saini na mamlaka hizo tarehe 3 mwezi huu wa Agosti na hatimaye nyaraka nyongeza zilizotiwa saini, zitaruhusu WFP kufanya kazi ya kuanzisha mchakato huru wa kuandikisha familia ambazo zinahitaji zaidi msaada.

Kwa mantiki hiyo WFP itarejesha mgao wa chakula baada ya sherehe za Eid El Haj na ikilenga kufikia watu 850,000 wenye mji mkuu Sana’a ambao haujapata msaada wowote wa chakula kutoka shirika hilo kwa miezi miwili sasa.

WFP imesema itaanza kugawa kadi za mfumo janja za kurahisisha mgao  huo kwa watu milioni 9 walioko maeneo yanayodhibiwa na mamlaka za Sana’a.

Akizungumzia hatua hiyo, msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi, Herve Verhoosel amesema,“tumepata hakikisho kutoka kwa wahouthi. Wahouthi wamekuwa wakijadiliana nasi kwa wiki chache zilizopita kupata nyaraka ambayo tumetia saini pamoja na muhimu zaidi ni kukubaliana vifungu vya kiufundi ambavyo tumetia saini jana.”

Bwana Verhoosel amesema kwamba wana kila sababu ya kuamini kuwa wahouthi wapo kwa maslahi ya wananchi na hivyo watawasaidia kutekeleza makubaliano hayo, “na bila shaka tutatathmini hali ilivyo kama mambo hayatakuwa hivyo.”

Makubaliano hayo yanaweka mfumo ambamo kwao utahakikisha kuwa operesheni hiyo ya WFP ambayo ni kubwa zaidi duniani  inatekelezwa kwa njia fanisi na kwa gharama nafuu.

Ni kwa mantiki hiyo, mamlaka zinazoshikilia mji wa Sana’a zimetoa andiko la hakikisho hilo kwa WFP ambapo shirika hilo litaweza kupeleka wafanyakazi wake na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya mchakato wa usajili wa wahitaji wa msaada wa chakula.

Wafanyakazi wa WFP na wadau wao watapatiwa ruhusa ya kufika maeneo yote wanayotaka kwenda bila vikwazo vyovyote.

Yemen inaongoza duniani kwa kuwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu ambapo mzozo wa zaidi ya miaka minne sasa u mesababisha mamilioni ya watu kukumbwa na njaa.

TAGS: Yemen, Sana’a, Houthi, Herve Verhoosel

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud