Tatizo la makazi laongeza adha kwa vijana wa LGBT:UN

9 Agosti 2019

Katika kuelekea siku ya kimataifa ya vijana , mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi dhidi ya machafuko na ubaguzi kwa misingi ya mwenendo wa kimapenzi au jinsia Victor Madrigal-Borloz, na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi Leilani Farha, wametoa wito kwa mataifa yote kuchukua hatua haraka ili kushughulikia vitendo vya kibaguzi dhidi ya vijana kutoka kundi la LGBT hasa linapokuja suala la nyumba au makazi.

Katika tarifa yao ya pamoja wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wamesema “ Kutokana na dini na utamaduni wa kutovumiliana ambao unajumuisha mwenendo wa kimapenzi na mifumo mingine ya ghasia, vijana ambao ni wasagaji, mashoga, watu wanaofanya mapenzi na jinsia zote, na waliobadili jinsia (LGBT) kote duniani wanakabiliwa na kutengwa kijamii na kiuchumi ikiwemo hata ndani ya nyumba zao, jamii zao, na familia zao kutoidhinisha. Na adhabu wakati mwingine zinawalazimisha kuondoka nyumbani hali ambayo inawaweka katika hatari zaidi ya kufanyiwa ukatili na ubaguzi.”

Wameongeza kuwa kama hiyo haitoshi ukilinganisha na umri waohali hiyo inachangia kwa wao kuwa tegemezi kiuchumi na pia kutegemea familia zao na mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa wataalm hao hii inaelezea ni kwa nini vijana wa LGBT ndio idadi kubwa ya watu wasio na makazi na kwa nini wakikosa makazi wanakumbwa na ubaguzi zaidi.

LGBTI wakiwa katika maandamano
OHCHR/Joseph Smida
LGBTI wakiwa katika maandamano

Hali ya kutokuwa na makazi wamesema wataalam hao inaweza kusababisha athari za mifumo mingine ya kutengwa dhidi ya haki za msingi za binadamu. Mfano mashuleni vijana wengi wa LGBT wanaonewa na kuwafanya wengi kuacha shule hali ambayo ina athari za muda mrefu katika maisha yao.

Kutokana hilo wamesema vijana wengi wa kundi hilo wako katika hatari ya kukosa kiwango cha elimu na ujuzi unaohitajika kupata ajira na kufikia kiwango bora cha kiuchumi hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kukosa fursa za kutafuta nyumba zinazostahili.

Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kuwa karibu theluthi mbili ya vijana wa LGBT wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na makazi hali iliyowasababishia pia matatizo ya afya ya akili, kwa mujibu wa utafiti wanakabiliwa na matatizo kama msongo wa mawazo, majaribio ya kutaka kujiua na kuwa na tabia mbili tofauti.

Pia wengi hukosa fursa za huduma za afya na wako katika hatari ya matumizi ya pombe kupita kiasi na utumiaji wa mihadarati.

Bendera za jamii ya LGBTI
UNAIDS (file)
Bendera za jamii ya LGBTI

Wataalam hao wamesisitiza kuwa chini ya sharia za kimataifa za haki za binadamu na katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs, serikali zina wajibu wa kutekeleza mara moja haki ya makazi na kushughulikia tatizo la kutokuwa na makazi.

Pia serikali zinapaswa kuchukua hatua mara moja na kutoa kipaumbele kushughulikia mizizi ya kutokuwa na makazi na kuitokomeza kabisa ifikapo 2030.

Kwa mantiki hiyo hatua zitakazopitishwa na kitaifa na kijamii serikali ni lazima zizuie vijana wa LGBT kukosa makazi na kuhakikisha será na sheria zote zinazohusu makazi zinajumuisha watu wa kundi hili na kutatua mahitaji yao mengine.

Siku ya kimataifa ya vijana huadhimishwa kila mwaka Agosti 12.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter