Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Homa ya nguruwe yatikisa uchumi wa nchi 6 barani Asia

Homa ya nguruwe ambayo inaambukiza sana na inaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji wadogo. (Maktaba Machi 2017)
IAEA/Laura Gil Martinez
Homa ya nguruwe ambayo inaambukiza sana na inaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji wadogo. (Maktaba Machi 2017)

Homa ya nguruwe yatikisa uchumi wa nchi 6 barani Asia

Afya

Ugonjwa wa homa ya nguruwe, ASF,  umeendelea kutikisa nchi za bara la Asia, ambapo kwa mwaka mmoja sasa tangu kubainika kwa ugonjwa huo takribani nguruwe milioni 5 wamekufa au wameteketezwa kutokana na kusambaa kwa gonjwa hilo hatari.

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linasema kwa sasa homa ya nguruwe ipo katika mataifa sita ambayo ni Camboda, China, Korea Kaskazini, Jamhuri ya watu wa Laos, Mongolia na Vietnam na hasara ambazo nchi hizo zimepata ni kupoteza asilimia 10 ya nguruwe walio nao.

Taarifa ya FAO iliyotolewa leo mjini Roma, Italia inasema kuwa ingawa ugonjwa huo unaonezwa kwa virusi si hatari kwa binadamu, bado unasababisha vifo miongoni mwa nguruwe kwa asilimia 100 na hivyo kusababisha hasara kuwab ya kiuchumi kwenye sekta hiyo ya nguruwe.

Ni kwa mantiki hiyo, Afisa mkuu wa afya ya wanyama FAO, Dkt. Juan Lubroth amesema wanashirikiana na mataifa mengine kwenye ukanda huo wa Asia ili kuepusha kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

“Kwa kuwa hakuna chanjo inayouzwa kukinga ugonjwa huo wa homa ya nguruwe, tunahitaji kuweka msisitizo kwenye harakati za kuzuia. Nchi lazima ziwe macho mipakani na kuzuia kuingia kwa wanyama au nyama au bidhaa nyingine za nguruwe zenye maambukizi,” amesema Dlt. Lubroth.


Homa ya nguruwe, ASF ilibainika kwa mara ya kwanza barani Afrika miaka ya 1920 ambapo hivi sasa ugonjwa huo pamoja na kulipuka barani Asia umeripotiwa pia barani Ulaya ambako hata hivyo kasi ya kusambaa ni ndogo miongoni mwa nguruwe pori.

Ugonjwa huu huambukizwa miongoni mwa wanyama hao iwapo nguruwe atakula chakula chenye damu ya nguruwe mwenye maambukizi au nyama ya nguruwe ambayo haijapikwa vizuri. Halikadhalika vifaa vya kazi vya wafugaji kama vile viatu, mavazi na vifaa vinginevyo vinaweza pia kueneza ugonjwa huo miongoni mwa nguruwe.

Nchini Vietnam, sekta ya nguruwe inachangia asilimia 10 kwenye mapato yatokanayo na sekta ya kilimo na nyama ya nguruweu ni robo tatu ya nyama yote inayoliwa nchini humo.

FAO inasema hadi sasa Vietnman imeshateketeza nguruwe milioni 3 katika harakati za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.