Kufikia SDG’s ni ndoto iliyo mbali kwa mamilioni ya vijana wa MENA:UNICEF

8 Agosti 2019

Ripoti iliyotolewa leo na shirikala Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF inasema endapo serikali hazitotoa kipaumbele katika masuala ya amani na utulivu na kuwekeza katika mambo muhimu kwa ajili ya Watoto na vijana katika ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika , MENA, basi kanda hiyo itashindwa kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030.

Hivyo ripota hiyo imetoa wito “wa kuchukua haraka hatua kuongeza matumizi ya huduma za awali za mtoto, ubora wa elimu, usawa wa kijinsia na ajira kwa vijana ili kuweza kufikia malengo hayo ya SDGs.”

Imesisitiza kwamba bila kuboresha elimu na kutoa fursa zenye maana basi kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini zitakabiliwa na hatari kubwa ya ongezeko la Watoto milioni 5 ambao hawatakuwa shuleni na zaidi ya asilimia 10 ya ongezeko la vijana wasio na ajira ifikapo mwaka 2030.

Hali halisi katika ukanda huo

Kwa mujibu wa ripota hiyo MENA Generation 2030, watoto na vijana katika ukanda huo ni Karibu nusu ya watu wote.

Na ukanda huo ndio wenye kiwango cha juu zaidi duniani cha ukosefu wa ajira kwa vijana ambapo huku kukiwa na wastani wa asilimia 40 miongoni mwa wasichana.

Ukanda wa MENA ni maskani ya Zaidi ya nusu ya wakimbizi wote duniani na ukiwa na Zaidi ya theluthi moja ya vijana wanaoishi katika hali tete na nchi zilizoathirika na vita.

UNICEF inasema “vijana katika eneo hilo wanahisi kuzidi kudorora kwa hali ya maisha katika muongo mmoja uliopita na nusu yao tu ndio wana Imani na serikali zao,.”

Karibu watoto milioni 15 hawaendi shulekutokana na mchanganyiko wa sababu zikiwemo umasikini, ubaguzi, kiwango dunia cha elimu, machafuko shuleni na vita.

Na miongoni mwa watoto walio shuleni nusu yao tu ndio wanaofikia kipimo kinachoangalia uwezo wa kusoma, hisabati na sayansi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud