Bima bunifu ya hatari ya mabadiliko ya tabianchi kusaidia Afrika:WFP

8 Agosti 2019

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yaandaa bima bunifu za hatari ya mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kuwalinda takriban watu milioni 1.3 Afrika Magharibu kutokana na janga la ukame.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la mpango wa chakula duniani WFP nchi zitakazofaidika na bima hiyo bunifu ni pamoja na Senegal, Mali, Maurotania, Burkina Fasso na Gambia.

Bima hizo zitatoa fedha za kusaidia jamii zisizojiweza ambazo ziko kwenye tishio kubwa la ukame kabla hali haijafikia kuwa janga kubwa.

Kwa ujumla bima hizo zitakazonunuliwa zinaweza kutoka jumla ya dola milioni 49.5 zitakazotumika katika nchi zote tano.

WFP na shirika la Start Network wamenunua bima hizo”Replica” za hatari ya mabadiliko ya tabianchi kutoka katika kitengo Muungano wa Afrika (AU) cha uwezeshaji wa kupambana na hatari Afrika (ARC) ili kusaidia bima kama hizo zilizonunuliwa na serikali husika.

Mradi huu ambao unajulikana kwa jina “ARC Replica” unaziruhusu serikali na mashirika ya misaada ya kibinadamu kupata fedha haraka na kuzifikisha kwa watu wasiojiweza wanaohitaji msaada wakati wa ukame mkubwa.

Kwa mujibu wa Silvia Caruso mkurugenzi wa WFP nchini Mali “ARC replica inaimarisha uwezo wa bima na kuongeza idadi ya watu watakaofaidika na malipo ya bima hiyo wakati wa janga kubwa la ukame.”

Ameongeza kuwa fedha hizo zitasaidia kulinda mifugo na samani zingine lakini pia program ya lishe hasa kwa watoto walio na utapiamlo.

Na ili kuhakikisha msaada unawafikia watu wanaouhitaji haraka Start Network na WFP wameshazungumza na serikali zinaopewa bima hizo ili kubaini jinsi gani fedha hizo na msaada vitafikishwa kwa walengwa.

Meneja mradi wa Benki ya maendeleo ya KfW Veronika Bertrama amesema “nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa na hatari ya majanga bila kujitayarisha ipasavyo. Na mara majanga yanayowakumba mara nyingi mashirika ya kibinadamu huenda kutoa msaada yakiwa yamechelewa na kuziacha jamii zilizoathirika katika hatari zaidi.”

Naye Bwana .Abdoulaye Noba mkurugenzi wa ulinzi wa kiraia na msimamizi wa program ya ARC nchini Senegal amesema “ARC Replica ni mradi bunifu unaoziwezesha nchi wanachama wa ARC na mashirika ya misaada ya kibinadamu kuchukua hatua haraka kukabiliana na majanga pindi yanapozuka kupitia mchakato wa ufadhili kama bima na malipo hufanyika haraka ndani ya wiki mbili tofauti na utamaduni wa kawaida wa mashirika ya misaada ambayo huchukua muda mrefu kubaini tatizo, na kutoa ombi la ufadhili ambapo mara nyingi fedha zinapopatikana maisha ya watu wengi yanakuwa yameshapotea na kusambaratika.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter