Heko Nyusi na Momade kwa makubaliano ya amani Msumbiji- Guterres

7 Agosti 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua iliyofikiwa nchini Msumbiji ya kutiwa saini kwa makubaliano ya amani na maridhiano kati ya chama tawala FRELIMO na kile cha upinzani, RENAMO.

Makubaliano hayo yalitiwa saini tarehe 6 mwezi huu wa Agosti kwenye mji mkuu Maputo kati ya Rais Filipe Nyusi na Rais wa RENAMO Ossufo Momade na yanahusisha kumaliza chuki na kuleta mabadiliko ya katiba na kupokonya silaha wapiganaji wa Renamo na hatimaye wajumuishwe kwenye vikosi vya usalama au maisha ya kiraia.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa hii leo jijini New York, Marekani na msemaji wake, amewapongeza Rais Nyusi na Bwana Momade kwa harakati zao za kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na azma yao ya kutamatisha mchakato wa amani.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wadau wote wa kitaifa kuchangia katika amani ya kudumu, maridhiano na utulivu kwenye taifa hilo ambalo punde tu baada ya uhuru mwaka 1975 lilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe hadi mwaka 1992.

Amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa katika kusaidia utekelezaji wa mkataba huo wa amani na kuleta mchakato ambao ni wa dhati na wenye maridhiano ya kudumu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Msumbiji.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter