Cheti pekee cha kifo kwa waliotoweshwa hakitoshi, tuonyesheni walipozikwa- Khoulani

7 Agosti 2019

Mkuu wa Idara ya siasa na masuala ya ujenzi wa amani, kwenye Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo amewaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama la umoja huo kuwa pande zote kwenye mzozo wa Syria zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kuwaachia bila masharti yoyote watu wanaoshikiliwa au waliotekwa nchini humo.

Akihutubia Baraza la Usalama hii leo Jumatano, lililokutana kujadili watu waliopotea au wanaoshikiliwa nchini Syria, Bi. DiCarlo amesema, “uwajibikaji vitendo vibaya zaidi vya ukiukwaji wa haki za binadamu na zile za masuala ya kibinadamu ni muhimu ili kufikia amani ya kudumu nchini Syria.”

Ameongeza kuwa, “ni kwa msingi huo, pande zote kwenye mzozo huo wa Syria ulioanza mwaka 2011 hususan serikali zinapaswa kushirikiana kikamilifu na tume ya kimataifa ya uchunguzi wa Syria, tume ambayo ni huru na haigemei upande wowote.”

Halikadhalika, msaidizi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa “kwa kuzingatia kuendelea kushindwa kufikia maeneo yanayoshikiliwa watu nchini Syria, Umoja wa Mataifa hauna takwimu rasmi za wale wanaoshikiliwa, waliotekwa au waliopotea. Kile ambacho Umoja wa Mataifa inafahamu kinatokana na maelezo yaliyorekodiwa na kuthibitishwa na Tume ya Uchunguzi kwa Syria iliyopatiwa mamlaka na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu tangu kuanza kwa mzozo mwaka 2011.”

Wakati Umoja wa Mataifa hauna uwezo wa kuthibitisha, ripoti zinadokeza kuwa zaidi ya watu 100,000 hadi sasa wanashikiliwa, au wametoweka au wamekamatwa ambapo kwa kiasi kikubwa wamefanyiwa vitendo hivyo na serikali ya Syria.

Bi. DiCarlo pia amesema ya kwamba, “wanawake, kando ya kuwa waathirika wa moja kwa moja, wamekumbwa na madhila kwa vitendo vya waume zao au marafiki zao wa kiume kutoweka. Wanawake wa Syria wanapoteza haki zao za kisheria, ikiwemo ya makazi, ardhi na kumiliki mali.”

Amesema ni katika mazingira hayo, wanawake wengi wanabeba mzigo wa kulea familia zao. “Kwa wakimbizi au wakimbizi wa ndani, changamoto hizi zinaongezeka maradufu,” amesema mkuu  huyo wa Idara ya siasa na ujenzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa.

Msitupatie tu vyeti vya vifo vya ndugu zetu, tupatieni na ripoti za sababu za vifo na mtuonyeshe na makaburi

Wakati wa kikao hicho, Amina Khoulani, ambaye kaka zake watatu walitekwa na serikali ya Syria kwa kushiriki maandamano ya amani amesema kuwa, “Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewaangusha siyo tu wasyria wanaoshikiliwa bali pia familia zao.”

Bi. Khoulani amesema, “ni wajibu wenu kuwalinda wasyria dhidi ya mfumo ambao unawaua, unawatesa au unaoshikilia raia wake kinyume cha sheria, na kukiuka sheria za kimataifa kama ilivyohitimishwa na ripoti ya kamisheni ya kimataifa ya uchunguzi dhidi ya Syria.”

“Mmeachia kura turufu na visingizio vyenu kuachia kile kilicho haki na sawa. Ni wajibu wenu kusaka njia ya kumaliza ukwepaji huu wa sheriana kutokomeza vitisho hivi,” amesema Bi. Khoulani.

Bi. Khoulani ni miongoni mwa waaanzilishi wenza wa taasisi ya Familia kwa ajili ya Uhuru, inayoongoza harakati za wanawake na ilizinduliwa mwaka 2017 na familia ambazo wapendwa wao wanashikiliwa au wametoweka.

Amina Khoulani, mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Families for Freedom, akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Syria. (7 Agosti 2019)
UN /Loey Felipe
Amina Khoulani, mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Families for Freedom, akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Syria. (7 Agosti 2019)

Hala, ambaye ni daktari na mwanzilishi mwenza wa taasisi hiyo naye pia alihutubia Baraza la Usalama akisema kuwa familia zimeumia sana na zimechoka kwa hiyo ni wakati wa chombo hicho kichukue hatua.

Amesema, “Baraza lazima lipitishe azimio la kushinikiza serikali ya Syria na pande zote kinzani ziweka bayana orodha ya wale wote wanaoshikiliwa sambamba na maeneo walipo na hali zao na kuacha mara moja kuwatesa.”

Hala ameenda mbali akisemakuwa, “kwa wale wanaoshikiliwa, cheti cha kifo pekee hakitoshi, ripoti ya sababu za kina za kifo na eneo la mazishi lazima ikabidhiwe kwa familia.”

Hata hivya mwakilishi wa Syria, Louay Fallouh amesema, “serikali yangu inakataa na kukanusha vitendo hivyo ambavyo amesema baadhi ya wajumbe wa Baraza wamekuwa wakitaja na kushushia hadi taifa langu.”

Amesema wajumbe hao ikiwemo Uingereza na Marekani hazina haki ya kisheria au haki ya kimaadili ya kuitisha kikao kinachoangazia masuala ya kibinadamu akisema kuwa, “nchi hiyo hadi leo hii zimekuwa zikishiriki moja kwa moja kuingilia nchi yangu.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter