Wahudumu wa afya wa kujitolea mashinani wasaidia kuimarisha unyonyeshaji watoto Kenya

7 Agosti 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF limesema mpango wa kupunguza utapiamlo na kuimarisha afya ya mama na mtoto nchini Kenya, umesaidia kuongeza kiwango cha unyonyeshaji watoto maziwa ya mama pekee. 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Kenya inaonyesha wanawake wakipatiwa mafunzo ya kunyonyesha watoto wao kliniki huku shirika hilo likisema kuwa kuboresha lishe ya mama na mtoto kumeongeza unyonyeshaji wa maziwa pekee ya mama kutoka asilimia 32 hadi 61 huku udumavu wa watoto ukipungua kutoka asilimia 35 hadi 26.

Hata hivyo UNICEF inasema pamoja na mafunzo ya kuandaa lishe bora kwa mama, bado watoto wachanga wanapatiwa si tu maziwa ya mama pekee bali vyakula vingine kama vile uji.

Hofu hiyo ikasababisha UNICEF kuwa na mpango wa kijamii wa kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya makuzi ya watoto kama anavyoelezea Miriam Chesire, mratibu wa lishe eneo la Koibatek kupitia video hii ya kwamba,“mpango huu unaelimisha akina mama jinsi ya kujitunza wao na watoto wao wakati wa ujauzito na unyonyeshaji. Kisha mtoto anafuatiliwa hadi anatimiza miaka mitatu. Tuliamua kufuata jamii mashinani kwa sababu si akina mama wote wanafika kliniki. Kuna wanawake wanajifungua nyumbani.”

UNICEF inasema mpango huo rafiki kwa mama na mtoto unauangaisha hospitali na jamii mashinani ambapo mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea kwa kufuatilia akina mama na mtoto mashinani ni Maimuma Hussein.

Hivi sasa UNICEF inasema kuwa jamii imehamasika na imebeba jukumu la afya yao tofauti na awali ambapo hawakuwa wamefikia jamii mashinani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud