Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Mbinu za kujengea jamii mnepo zinahitajika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika-FAO

Mkulima karibu na mji wa Kisumu nchini Kenya akilima shamba lake.
World Bank/Peter Kapuscinski
Mkulima karibu na mji wa Kisumu nchini Kenya akilima shamba lake.

 Mbinu za kujengea jamii mnepo zinahitajika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika-FAO

Tabianchi na mazingira

Mbinu za kujengea jamii mnepo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima ziimarishwe, wamesema washiriki wa mjadala wa ngazi ya juu kuhusuuhakika wa upatikanaji wa chakula  Afrika ulioandaliwa na serikali ya Rwanda mjini Kigali kwa ushirikiano na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, kamisheni ya Muungano wa Afrika, Benki ya maendeleo Afrika, mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD  na Benki ya Dunia. Taarifa zaidi na Arnold Kayanda.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Maria Helena Semedo amesema, “wakulima kwa muda mrefu wamekuwa ni wabunifu, wanachohitaji ni sera ambazo zinawalinda na kuwajengea mnepo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Wanahitaji kupata tarifa kuhusu teknolojia na uwekezaji na wanapaswa kushirikishwa katika mjadala kuhusu ubunifu.”

Kwa mujibu wa taarifa ya FAO sekta ya chakula na kilimo ni miongoni mwa sekta zilizo hatarini zaidi kwa athari mbaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi huku wakulima wadogo wadogo, na wajarasiliamali na familia zao ambao hutegemea kilimo kitokancho na mvua wanakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi.

FAO inasema , njaa imeongezeka katika nchi nyingi za bara Afrika na hivyo kulifanya bara hilo kuwa bara lililo na idadi kubwa ya watu wasio na lishe bora ikiwa ni asilimia 20, hali ambayo inasababisha na mizozo na mabadiliko ya tabianchi hususan Afrika mashariki ambako asilimia 30.8 ya watu ikiwa ni sawa na watu milioni 133 wanakabiliana na changamoto ya lishe toshelezi.

Kongamano limejulishwa kwamba inawezekana kukabiliana na athari hizo kwa kutumia hatua madhubuti zikilienga kujengea jamii mnepo.

Jana Jumatatu, washiriki wa kongamano walipitisha makubaliano ya kusaidia nchi za Afrika katika hatua  zake za kuimarisha uhakika wa chakula ambapo kujengea jamii mnepo ni baadhi ya vipaumbele vya FAO barani Afrika dhidi ya changamoto mbali mbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi kama kiungo muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu hususan katika changamoto ya kulisha watu bilioni 2 Afrika ifikapo mwaka 2050

Dhamira ya kongamano hilo la viongozi kuhusu chakula na uhakika wa chakula Afrika ni kuwezesha majadiliano kati ya serikali na wadau muhimu wa maendeleo katika hatua za kuimarisha kilimo na mifumo ya chakula Afrika ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Takriban watu 250 wanashiriki kongamano hilo la siku mbili linalomalizika leo, akiwemo Rais wa Rwanda, Paul Kagame na kamishna wa Ulaya kwa ajili ya ushrikiano na maendeleo kimataifa, Neven Mimica.