Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Melisa Fleming ndio mkuu mpya wa idara ya mawasiliano ya kimataifa UN

Melissa Fleming (kushoto) alipokuwa msemaji na mkuu wa mawasiliano wa UNHCR, akimuhoji Fabrizio Hochschild, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mikakati na uratibu.
UNHCR/Susan Hopper
Melissa Fleming (kushoto) alipokuwa msemaji na mkuu wa mawasiliano wa UNHCR, akimuhoji Fabrizio Hochschild, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mikakati na uratibu.

Melisa Fleming ndio mkuu mpya wa idara ya mawasiliano ya kimataifa UN

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amemteua Melissa Fleming raia wa Marekani kuwa ndio mkuu mpya wa idara ya mawasiliano ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa au DGC. Bi. Fleming anachukua wadhifa huo wa msaidizi wa Katibu mkuu akimrithi Alison Smale raia wa Uingereza ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa uwajibikaji wake na huduma kwenye shirika la Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa ya uteuzi huo Katibu Mkuu amesema Bi. Fleming anakuja katika kazi hiyo na uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ya maono ya kimkakati, uongozi wa ubunifu na utaalam wa mawasiliano katika nyanja mbalimbali za mashirika ya kimataifa kuanzia haki za binadamu, hatua za masuala ya kibinadamu, kuzuia mizozo, ujenzi wa amani, vyombo huru vya habari na kupinga kuenea kwa uzalishaji wa nyuklia, usalama na ulinzi.

Tangu 2009 ameshika wadhifa wa mkuu wa mawasiliano ya kimataifa na msemaji wa  ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi (UNHCR) huko Geneva Uswis. Akiwa UNHCR Bi. Fleming aliongoza kampeni za kufikia vyombo vya habari vya kimataifa, ushiriki wa mitandao ya kijamii na huduma kwa vyombo mbalimbali vya habari ya media vinavyohudumia wafuasi tofauti kuanzia vyombo vya habari, umma, wafadhili, serikali na wakimbizi wenyewe.

 Melissa Fleming
Picha na UNHCR/Jean-Marc Ferré
Melissa Fleming

 

Bi Fleming alijiunga na UNHCR akitokea Shirika la kimataifa la nishati ya Atomiki (IAEA), ambapo alihudumu kwa miaka nane kama msemaji na mkuu wa kitengo cha Habari na mawasiliano. Kabla ya IAEA, aliongoza timu ya wanahabari na mawasiliano ya umma katika shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya  (OSCE).

Pia aliwahi kuwa  mtaalam wa masuala ya umma katika Redio Free Europe na radio Liberty huko Munich nchini Ujerumani , baada tu ya kuanza kazi yake kama mwandishi wa habari. Kuanzia mwaka wa 2016 hadi 2017, aliwahi kuwa mshauri mwandamizi na msemaji wa timu ya mpito ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa anaingia.

Bi Fleming ana stashahada ya uzamili katika masuala ya Sayansi katika Uandishi wa habari kutoka chuo kikuu cha mawasiliano, cha Boston na pia ana Shahada ya Sanaa katika Mafunzo ya Kijerumani kutoka Chuo cha Oberlin.