Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliomjeruhi mtoto mpalestina Abdul Rahman Shteiwi wafikishwe mbele ya sheria- OHCHR

Mtoto wa umri wa miaka 12 akipita pembezoni mwa nyumba iliyobomolewa na mashambulizi kutoka angani yaliyofanywa na Israeli katika jiji la Rafah, kusini mwa Gaza mwaka 2012.
UNICEF/UNI132737/El Baba
Mtoto wa umri wa miaka 12 akipita pembezoni mwa nyumba iliyobomolewa na mashambulizi kutoka angani yaliyofanywa na Israeli katika jiji la Rafah, kusini mwa Gaza mwaka 2012.

Waliomjeruhi mtoto mpalestina Abdul Rahman Shteiwi wafikishwe mbele ya sheria- OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, OHCHR, kupitia msemaji wake Rupert Colville imesema inasikitishwa sana na hali ya mtoto mpalestina Abdul Rahman Shteiwi  ambaye alipigwa risasi kichwani na vikosi vya usalama vya Israel (ISF) mnamo tarehe 12 ya mwezi huu wa Julai katika kile kinachoonekana kuwa mfano wa matumizi makubwa ya nguvu.

Colville amesema ingawa kumekuwa na ripoti kuwa vikosi vya ulinzi vya Israel vimeanza uchunguzi wa ndani, “tunatoa wito kwa mamlaka za Israel kufanya uchunguzi wa kina, wa hakika, usioegemea upande wowote na ulio huru kuhusu tukio hili na kuhakikisha kuwa waliohusika na utekelezaji wa jambo lolote baya wanawajibishwa.”

Tukio hilo lilitokea katika maandamano ya kila wiki katika kijiji cha Kafr Qaddum karibu na Nablus.

OHCHR inasema kuwa ni katika wakati ambapo waandamanaji walikuwa wakichoma matairi na kurusha mawe kwa vikosi vya usalama vya Israel,  baada ya askari wa Israel ya kurusha risasi za mpira na mabomu ya kutawanya watu, ndipo inaripotiwa waligeuka na kuanza kutumia risasi za moto bila sababu za msingi za kutumia nguvu ya ziada.

Bwana Colville ameeleza kuwa kulingana na vyanzo kadhaa vya uhakika, mtoto huyo wa miaka tisa, Abdul Rahman alikuwa hashiriki katika maandamano. Inaripotiwa kuwa alikuwa mita 100 mbali ya vurugu zilizokuwa zinaendelea na hakuna namna ambavyo alikuwa anahatarisha maisha ya wanajeshi hao.

Risasi aliyopigwa kichwani mtoto huyo imesababisha tundu kubwa na mipasuko kadhaa katika fuvu lake. 

Awali alipelekwa katika hospitali iliyoko Nablus na kisha baadaye akahamishiwa katika hospitali ya Israel ambako pamoja na kuwa amesalia kuwa hai lakini inasemwa yuko katika hali mbaya. 

Uchunguzi unaonesha kuwa kumetokea madhara kadhaa katika kichwa cha mtoto huyo hali inayoathiri ubongo wake na kumweka katika uwezekano wa kutorejea katika hali yake hata kama atapona.

“Watoto wanatakiwa kupewa ulinzi maalumu. Hawatakiwi kulengwa na hawatakiwi kuwekwa katika hatari ya machafuko au kuhamasishwa kushiriki katika vurugu,” amesema msemaji huyo wa OHCHR.