Ripoti ya mwaka 2018 yaonesha idadi kubwa ya watoto waliuawa na kukatwa viungo

30 Julai 2019

Mwaka 2018 umeongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto waliouawa au waliokatwa viungo kwenye maeneo ya mizozo tangu Umoja wa Mataifa uanze kufuatilia na kuripoti uhalifu mkubwa kwenye vita, imesema ripoti iliyotolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa ujumla kumekuwa na visa 24,000 vya ukatili ambavyo vimethibitishwa mwaka 2018 katika maeneo 20 yanayoshuhudia mizozo katika ajenda ya watoto kwenye mizozo.

Ripoti imesema huku idadi ya vitendo vya ukiukaji vya aina nyingine vikipungua au kusalia viwango vya awali, watoto zaidi ya 12,000 waliuawa au kujeruhiwa mara nyingi na matukio na ufyatulianaji risasi, mabomu ya kutegwa, vilipuzi vya mabaki ya vita, mabomu ya kutegwa ardhini na vitendo vya kijeshi kutoka kwa vikosi vya taifa, visivyo vya taifa na vile vya kiamtaifa.

Akizungumzia ripoti hiyo wakati akiwasilisha  mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya silaha Bi. Virginia Gamba amesema, “inasikitisha sana kwamba watoto wanaendelea kuathirika vibaya na uhalifu wa silaha na inasikitisha kuwaona wakiuawa au kuachwa na kulemazwa kutokana na uhasama.”

Bi. Gamba ameongeza kwamba, “ni muhimu kwamba pande husika katika mizozo ziweke kipaumbele katika ulinzi wa watoto. Hili haliwezi kusubiri, pande husika katika mizozo lazima zichukue wajibu wa kulinda watoto na kuweka mikakati ya kuhakikisha uhalifu huu.”

 Ripoti imetanabaisha baadhi ya vitendo vya uhalifu dhidi ya watoto huku watoto takriban 7,000 wakitumikishwa jeshini huku Somalia ikisalia kuwa nchi yenye idadi kubwa ya watoto waliotumikishwa jeshini ikifuatiwa na Nigeria na Syria.

Kwa mujibu wa ripoti, kumeripotiwa visa 933 vya ukatili wa kingono dhidi ya wavulana na wasichana, idadi hii ikikadiriwa kuwa ndogo kuliko idadi kamili kutokana na ukosefu wa ufikiaji, hofu dhidi ya unyanyapaa na kushambuliwa.

Kwa upande mwingine  mashambulizi dhidi ya shule na hospitali yamepungua kwa ujumla lakini yameimarika katika baadhi ya maeneo hususan Afghanistan, Syria ambako kuna mashambulizi hayo tangu kuanza kwa mzozo nchini.

Mali ni mfano wa matukio ya watoto kunyimwa haki ya kupata elimu na kutumikishwa jeshini huku shule 827 zilifungwa nchini Mali kufikia mwisho wa mwezi Desemba mwaka  2018, na kuwanyima watoto 244,00 fursa ya kupata elimu.

Kuzuiliwa na kuachiwa kwa watoto waliohusishwa kwenye mizozo

Ripoti inasema badala ya watoto kuchukuliwa kama wahanga wa utumikishwaji, maelfu ya watoto kote ulimwenguni walizuiliwa kwa uhusiano wao au madai ya uhusiano na vikundi vilivyojihami mwaka 2018.

Katika muktadha huo ripoti imetoa wito kwa mataifa kufanya kazi na Umoja wa Mataifa kuwatafuta watoto na wanawake wanaodaiwa kuhusika na makundi ya waasi huku msingi ukiwa ni mahitaji ya mtoto yakipewa kipaumbele.

Idadi ya watoto walionufaika na msaada wa kujumuishwa katika jamii imeongezeka mwaka 2018 kutoka 13,600 kutoka 12,000 mwaka 2017 ambapo ripoti imependekeza kuimarishwa kwa ufadhili ili kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka huku watoto wengi wakitenganishwa na makundi yaliojihami.

Jambo lingine lililoripotiwa ni kuhusu kutiwa saini kwa  mpango wa hatua tatu kwa ajili ya kuzuia ukatili na kulinda watoto ikiwa ni kufuatia mazungumzo na pande husika katika mzozo mwaka 2018 ukihusisha nchi mbali mbali ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako makundi yaliyaojihami mawili yalitia saini makubaliano ya hatua na Syria ambako vikosi vya kidemokrasia Syria waliridhia makubaliano hayo.

Halikadhalika hatua zimepigwa pia katika ulinzi wa watoto na kutokomeza utumikishwaji wa watoto nchini Yemen na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amekumbusha pande husika kwenye mzozo kuhusu wajibu wao wa kulinda raia akiongeza kwamba ni lazima, “wajizuie kwenye mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya raia wakiwemo watoto,” pia amekumbusha kwamba, “amani inasalia kuwa njia mujarabu ya kulinda watoto walioathirika na migogoro ya silaha.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter