Usafirishaji haramu wa binadamu ni dondandugu la kila nchi-UN

30 Julai 2019

Usafirishaji haramu wa binadamu ni uhalifu mbaya kabisa na unagusa kila pembe ya dunia, huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake, wasichana na watoto umesema leo Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu na madawa UNODC ,katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu, asilimia 72 ya waathirika wa uhalifu huu ni wanawake na wasichana huku idadi ya watoto waliothirika ikiongezeka mara mbili tangu mwaka 2004 hadi 2016.

 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa asilimia kubwa ya waathirika husafirishwa kwa minajili ya kwenda kutumiwa katika biashara ya ngono, kufanyishwa kazi kwa shuruti, watoto kuingizwa jeshini kama wapiganaji na mifumo mingine ya unyanyasaji na ukatili.

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema vita, watu kutawanywa, mabadiliko ya tabianchi, ubaguzi , majanga ya asili na umasikini  ndio vinawachochea wasafirishaji haramu kutumia fursa ya zahma hizo kuendeleza biashara zao za kihalifu, na sasa wahamiaji nao ni walengwa wakubwa wengi wakipoteza maisha mikononi mwa wasafirishaji hao haramu baharini na hata nchi kavu wakitaka kwenda kusaka mustakbali bora ughaibuni.

Guterres ameongeza kuwa hatua za pamoja zimesaidia kwa kiasi fulani ikiwemo mkataba wa Palermo wa kuzuia, kukomesha na kuwaadhibu wasafirishaji haramu wa binadamu hususani wanawake na watoto na kwamba nchi nyingi zimeweka sheria na hata kutoa hukumu dhidi ya wahalifu hao, lakini bado hatua zaidi zinahitajika ili kuifikisha mitandao ya kimataifa ya usafirishaji haramu kwenye mkono wa sheria na kubwa zaidi kuhakikisha waathirika wanatambulika, kupata ulinzi na huduma zinazohitajika.

Na amezitaka nchi zote na kila mtu kuchukua hatua kuhakikisha uhalifu huu unakomeshwa na waathirika kusaidiwa kujenga upya maisha yao. Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika na uhalifu huu na waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Kangi Lugola amesema serikali imelivalia njuga kwa hatua madhubuti

(SAUTI YA KANGI LUGOLA)

Naye Enna mwenyekiti wa kamati ya kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu katika shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM Tanzania ambaye anafanya kazi kwa karibu na serikali katika vita hivyo anasema

(SAUTI YA ENNA…)

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter