Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko makubwa yanahitajika kuwajumuisha wahanga wa usafirishaji haramu-Mtaalam UN

Msichana akijipodoa katika dangura mji wa Tangail nchini Bangladesh. Mwanamume alwaahidi kuwatafutia kazi lakini badala yake akawauza Kandapara.(2009)
© UNICEF/UNI91025/Noorani
Msichana akijipodoa katika dangura mji wa Tangail nchini Bangladesh. Mwanamume alwaahidi kuwatafutia kazi lakini badala yake akawauza Kandapara.(2009)

Mabadiliko makubwa yanahitajika kuwajumuisha wahanga wa usafirishaji haramu-Mtaalam UN

Haki za binadamu

Kuelekea siku ya kupinga usafirshaji haramu wa watu, mtaaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu usafiri haramu wa watu, hususan wanawake na watoto, Maria Grazia Giammarinaro, amehimiza mataifa kuimarisha juhudi kuhakikisha fidia kwa watu ambao wanasafirishwa kiharamu.

Mtaalam huru huyo kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi amesema, “ni muhimu sana kwamba mataifa yawekeze katika suluhu za muda mrefu ili kuhakikisha ujumuishwaji wa kijamii kwa waathirika wa usafirishwaji haramu wa binadamu. Hii inamaanisha kwamba kuna utaratibu wa nchi kuhakikisha waathirika wanaweza kupata haki na mbinu za kufidiwa."

Bi. Giammarinaro amesema mabadiliko makubwa yanahitajika katika nchi kwa ajili ya kushughulika suala la uhamiaji na usafirishwaji haramu.

Ameongeza kwamba, “sera kandamizi na zinazoelekeza chuki dhidi ya  wahamiaji na wahamiaji kuchukuliwa kama wahalifu pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa msaada wa kibinadamu haviendani na hatua mujarabu dhidi ya usafishajim haramu.”

 Halikadhalika mtaalam huru huyo ametoa angalizo dhidi ya wanasiasa wanaoeneza chuki na kujenga kuta, kuruhusu kuzuiwa kwa watoto na kutoruhusu wahamiaji walio hatarini kuingia katika nchi mwao akisema kwamba, “wanafanya kinyume na mahitaji ya nchi yao.”

Bi. Giammarinaro amesema kile ambacho kinahitajika ni uhamiaji kwa utarataibu ambao unajumuisha kuweka mikakati kuwajumuisha wahamiaji kijamii kwani hili ni muhimu pia kwa wahanga wa usafirishaji haramu, ikiwemo wanawake ambao wanakabiliwa na ubaguzi, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji na watoto ambao wanakabiliwa na hatari ya unyanyasaji wakati wa  safari zao hususan wanaposafiri pekee yao.

Mtaalam huru huyo ametoa wito kwa nchi kutoa vikwazo vinavyowazuia wahanga wa usafirishaji haramu kupata haki na kuwapa uhifadhi watu walioathirika na kuhakikisha kwamba hawazuiliwai au kushtakiwa kwa vitendo vya uhalifu ambavyo huenda walifanya kutokana na hali yao ya kusafirishwa kiharamu. Na iwapo wamehukumiwa, rekodi za uhalifu zinapaswa kufutwa.