Muarobaini wa adha ya madarasa Côte d'Ivoire ni taka za plastiki:UNICEF

29 Julai 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa ushirikiano na kampuni ya biashara ya kijamii ya Colombia Conceptos Plasticos, leo wametangaza kuzindua kiwanda cha kwanza cha aina yake ambacho kitabadilisha taka za plastiki zilizokusanywa nchini Cote d'Ivoire na kuzifanya kuwa matofali ya kawaida ya plastiki ya gharama nafuu na yanayodumu kwa muda mrefu, ambayo yatatumika kujenga vyumba vya madarasa vinavyohitajika sana katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Akizungumzia hatua hiyo mkurugenzi mkuu wa UNICEF Henrietta Fore amesema“kiwanda hiki kitakuwa cha aina yake na cha kisasa kinachojali mazingira na kuwa suluhisho nzuri la  hatari na changamoto kubwa za kielimu ambazo zinawakabili watoto wa Afrika na jamii zao. Na umuhimu wake ni mkubwa  ambao ni maradasa zaidi kwa watoto nchini Côte d’Ivoire, kupunguza taka za plastiki katika mazingira, na kuongeza kipato kwa familia nyingi masikini.”

Kwa mujibu wa UNICEF Côte d'Ivoire inahitaji madarasa  15,000 ili kukidhi mahitaji ya watoto wasio na mahali pa kusomea. Na ili kuziba pengo hilo UNICEF imeingia ubia na Conceptos Plasticos kutumia taka za plastiki zilizokusanywa katika maeneo mbalimbali mjini Abidjan kwa ajili ya kujenga madarasa 500 yatakayotumiwa na watoto zaidi ya 25,000  walio na mahitaji ya haraka katika kipindi cha miaka miwili ijayo lakini pia kukiwa na uwezekano mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa tofali hizo na ujenzi wa mdarasa zaidi.

Wabia hao wamesema mara tu kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi kikamilifu kitakuwa na uwezo wa kubadili tani 9,600 za taka za plastiki na kuwa matofali kila mwaka , hatua ambayo itakuwa chachu kubwa ya kipato hasa kwa wanawake wanaoishi katika umasikini watakaoingia katika biashara hiyo.

Hadi sasa kampuni ya Conceptos Plasticos inasema madarasa tisa yameshajengwa

Gonzagueville, Divo na Toumodi kwa kutumia matofali ya plastiki yaliyotengenezwa Colombia ili kuonyesha mfano wa jinsi ya kuyatengeneza na kuyatumia matofali hayo.

UNICEF inasema“matofali hayo kwa asilimia 100 yanatengenezwa na plastiki na hayaungui moto gharama zake ni asilimia 40 chini ya tofali za kawaida na uzito wake ni asilimia 20 mepesi zaidi ya tofali za kawaida na pia yatadumu mamia ya miaka zaidi ukilinganisha na tofali za kawaida. Kwa kuwa ni plastiki matofali haya hayapitishi maji, na yametengenezwa ili kuhimili upepo mkali.”

Hivyo mbali ya kwamba yatatatua adha ya madarasa Côte d’Ivoire, yatawatoa watu wengi katika umasikini na yatakuwa yanalinda mazingira.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter