Heko Rwanda kwa maandalizi bora ya kupambana na Ebola

25 Julai 2019

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani Dkt. Tedross Adhamon Ghebreyesus leo ameipongeza Rwanda katika juhudi zake za maandalizi ya kukabiliana na Ebola zinazoendelea na kuthibitisha kwamba hakuna kisa cha Ebola kilichoripotiwa nchini humo hadi sasa.

Bwana Tedross amesema “Rwanda imekuwa msitari wa mbele na kujitoa kimasomaso katika maandalizi ya kupambana na Ebola katika ngazi zote tangu mlipuko wa Ebola ulipoanza katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Tunapongeza hatua zilizochukuliwa hadi sasa na kuthibitisha kwamba hakuna kisa chochote cha Ebola Rwanda hadi sasa licha ya kiwango cha juu cha watu kusafiri baina ya nchi hizo mbili.”

Rwanda imeandaa mkakati wa kitaifa wa maandalizi na inatoa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu kubaini mapema na kukabiliana na ugonjwa wa ebola , pia inatoa elimu kwa jamii kuhusu Ebola, kutoa chanjo kwa wahudumu wa afya walio katika maeneo yenye hatari kubwa ya ebola , kutoa vifaa muhimu kwa vituo vya afya na kuendesha majaribio ya kupambana na na ugonjwa huo kana kwamba umezuka.

Zoezi la kuwapima na kuwachunguza watu kuhusu dalili za Ebola kwenye maeneo ya mpakani lilianza tangu mwanzo wa mlipuko DRC na limekuwa likiendelea tangu kusambaa kwa tarifa za kisa cha Ebola mjini Goma. Maelfu ya watu huvuka mpaka kila siku kutoka mji wa Gisenyi Rwanda na kuingia Goma na watu hao hupimwa joto la mwili, kunawa mikono  na kusikiliza ujumbe kuhusu ebola.

Kituo cha matibabu ya Ebola kimefunguliwa Rwanda na vitengo vingine 23 vimeandaliwa katika hospital mbalimbali kwenye wilaya 15 na majaribio ya kupambana na Ebola yamekuwa yakiendeshwa katika hospital ya kijeshi ya Kanombe, hospital ya Wilaya ya Gihundwe, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kamembe na kwenye kituo cha matibabu ya Ebola cha Rugerero ili kupima uwezo wa maandalizi ya Rwanda katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola, ambayo yatajumuisha huduma za dharura, ufuatiliaji, udhibiti wa visa na vipimo vya maabara.

Hadi sasa wahudumu wa afya 3000 wameshapewa chanjo dhidi ya Ebola katika maeneo ambayo yako hatarini , ikiwa ni hatua za kuzuia ikiwemo wahudumu zaidi ya 1100 kwenye mkoa wa Gisenyi.

Mkuu wa WHO amesema “Rwanda imewekeza kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya kupambana na ebola, lakini endapo mlipuko unaendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, kuna hatari kubwa ya kusambaa katika nchi jirani. Tunaitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kusaidia kazi hii muhimu ya kudhibiti ebola."

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud