Mradi wa UNICEF wa vitabu za kidijitali zatoa fursa kwa watoto wanoishi na ulemavu Kenya

24 Julai 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wamezindua jaribio la kitabu cha kidijitali katika shule 25 za msingi  nchini Kenya kwa lengo la kuimarisha elimu ya kidijitali hususan kwa watoto walio hatarini au maeneo ya vijijini au mitaa ya mabanda na wanaoishi na ulemavu. 

Kupita video ya UNICEF tunakutana na mwanafunzi wa shule ya msingi akiwa darasani amevalia sare ya shule ambayo ni sweta ya kijani na shati jeupe. Kwenye dawati ana kompyuta ndogo kwa makini kabisa anafuata maelekezo kupitia lugha ishara.

UNICEF imesema watoto wengi walio na ulemavu wa viungo mara nyingi wanakosa elimu kwa sababu ya kukosa vifaa elimu lakini vitabu mtandaoni ni habari njema. 

Vitabu hivi vinahakikisha kwamba watoto walio na ulemavu wa kuona wanapata vitabu hivyo kwa njia ya sauti na lugha nyepesi kwa walio na ulemavu wa upungufu wa kuelewa pia lugha ishara kwa viziwi. 

Mfumo huu unakaribishwa pia na walimu kama anavyosema mwalimu Martha Mwango kutoka shule ya msingi ya Aga Khan ambaye anaonekana na wanafunzi wake darasani

(Sauti ya Martha)

“Mfumo wa kidijitali wa kusoma ni mzuri sana kwa viziwi, ni wazo zuri ambalo tunalitekeleza kwa sababu wanafunzi hawa wanatumia uwezo wao wa kuona wakati wanasoma na vitabu vya kidijitali vina picha, ishara na rangi kwa hiyo inawatia moyo sana.”

Mfumo huu umetajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wanakwenda sambamba na wenzao wasio na ulemavu wa viungo kwani katika zama za sasa teknolojia inatumika katika mambo mbali mbali.

Kwa upande wao wanafunzi ambao walikuwa wamezoea mfumo wa kizamani wa mafunzo sasa wanapata taswira kamili kwani wanajifunza kupitia picha na video. Mwanafunzi Keith kupitia lugha ishara anasema, “nimependa sana kitabu hiki, ninafurahi kukisoma, ninapenda picha na kusoma hadithi zilizomo.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud