Joto la kupindukia laendelea kutamalaki Ulaya na Marekani-WMO

23 Julai 2019

Joto la kupindukia laendelea kulikumba bara Ulaya kwa wiki nyingine , huku kiwango cha joto kikivunja rekodi limesema shirika la hali ya hewa duniani WMO.

Kwa mujibu wa shirika hilo Jumatano na Alhamisi iliyopita joto hilo lilifurutu ada huku sehemu nyingi za Ulaya zikishuhudia viwango vya juu vya joto, jua Kali la kupita kiasi na fukuto la hali ya juu.

Mathalani Ujerumani na Benelux zilishuhudia rekodi mpya ya joto siku ya Alhamisi ambalo lilifika nyuzi joto 40°C.

WMO inasema juma hili pia limeanza kwa wiwango vya juu vya joto na jana Jumatatu usiku Ufanransa iliripotiwa kuwa na viwango vipya vya chini vya joto hususani kwenye maeneo ya Kusini Magharabibi ambako mji kama Bordeaux ukiwa na kiwango cha chini cha nyuzi joto 24.8°C na Toulouse nyuzi joto za chini ni 24.6°C .

Sehemu kubwa ya Ufaransa na Uswis imewekwa katika tahadhari ya joto kali daraja la 3 kwa siku nne mfululizo ikimaanisha kwamba watapata kiwango kikubwa kabisa cha joto kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.

Shirika hilo la utabairi wa hali ya hewa duniani limeongeza kuwa mbali ya Ulaya baadhi ya sehemu za Mashariki mwa Marekani zimeshuhudia joto la kupindukia mwishoni mwa wiki na maeneo mengi akijiwekea rekodi mpya ya joto lililofikia nyuzi 100°F sawa na nyuzi joto 37.8°C namaeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Atlantic City,  New jersey na uwanja wa ndege wa kimataifa wa JFK New york.

Na kituo cha kitaifa cha huduma za hali ya hewa Marekani mjini Omaha kilifanya majaribio ya kuoka biskuti kwenye gari ili kupima kiwango cha joto na baada ya saa 8 juani biskuti ilikuwa imeiva ikidhihirisha joto na jua lilikuwa Kali kiasi gani pia WMO inasema jaribio hilo linadhihirisha hatari iliyopo dhidi ya kuwaacha watoto au wanyama wafugwao kwenye gari katika kipindi hiki hata kama ni kwa muda mfupi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud