Matendo ya nchi nyingine yanayosababisha mabadiliko ya tabianchi, yanatuathiri sisi tusio na hatia-Msumbiji

22 Julai 2019

Miezi minne baada ya vimbunga viwili kikubwa kuipiga Msumbiji, WFP inadhihirisha kuwa gharama za mabadiliko ya tabianchi ni mbaya. Tathimini ya chakula ya hivi karibuni inaonesha kuwa watu milioni 1.6 wako hatarini kukosa chakula angalau kufikia mwezi septemba mwaka huu wa 2019. Hata hivyo WFP inajaribu kupambana na kupitia video yake mpya, shirika hilo linaonesha hali halisi ili kuwachagiza wadau kunyoosha mkono na kusaidia.

Video hii mpya ya WFP inaanza na mji ulioathirika zaidi wa Beira na viunga vyake. Kimbunga kiliyaharibu hata magari yaliyoachwa nje ya makazi yaliyotelekezwa.

Minda Guisado anajaribu kuokoa kile anachoweza kutoka katika nyumba yake ya zamani iliyoharibiwa katika kimbunga Idai. Ana umri wa miaka 34, na ni mjane anayewalea watoto watatu pamoja na mama yake. Maafisa wa serikali wa eneo hilo wanasema nyumba yake ya zamani iko katika eneo la mafuriko hivyo wamempatia kipande kidogo cha ardhi ili aishi na kulima katika makazi ya kuhifadhi waathirika wa mafuriko kilomita kadhaa kutoka katika eneo lake la awali.

(Sauti ya Minda Guisado)

 “Ghafla paa liliondoka na nyumba ikawa kama vile iko baharini. Kulikuwa na mawimbi ndani ya nyumba.”

Katika kambi ya Bairro Unidade, video iliyopigwa kutoka angani inamwonesha mwanaume mmoja akisukuma pikipiki katika barabara iliyofurika maji baada tu ya kimbunga Idai kupiga mnamo mwezi Machi tarehe 14 mwaka huu wa 2019 na kuwaacha watu milioni 1.7 wakiwa katika uhitaji mkubwa wa chakula na hekta 400,000 za mazao zikikadiriwa kusombwa na mafuriko wiki chache tu kuelekea msimu wa mavuno kati ya mwezi Aprili na Mei.

Kimbunga pia kilifanya uharibifu katikati mwa mji wa Beira. Nyumba nyingi na majengo bado hadi leo hazina  paa.

Meya wa Beira, Daviz Simango, kutokea katika jingo la manispaa ya Beira anaonesha majengo yaliyoharibiwa na kimbunga.

(Sauti ya Daviz Simango)

“Huu ndio uhalisia wetu. Watu sasa wanateseka. Wanahitaji kujenga upya makazi yao. Wengi wao hawana vipato vya kufanya hivyo.”

Meya Simango akizungumiza nchi zinazochangia katika mabadiliko ya tabianchi anasema,

(Sauti ya Daviz Simango)

“Wanatakiwa kubadili tabia zao. Wanatakiwa kuelewa kuwa kinachotokea katika upande wao kinatuathiri sisi hapa…watu tusio na hatia. Na sasa tunaomba rasilimali kutoka kwao ili kujijenga upya lakini rasilimali hizo hazijatufikia bado. Kwa hivyo hawaelewi kuwa mabaya wanayoyafanya upande ule, wanaua watu katika upande mwingine.”

WFP inasambaza chakula kwa watu wasio na makazi ambao walipoteza makazi yao katika kimbunga Idai. Takribani familia 300 zinaishi katika kambi. Wanapatiwa vipande vidogo vya ardhi kuzalisha chakula na wengi wameanzisha biashara zao.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter