Ni pigo kubwa kwetu kuondokewa na Yukiya Amano:IAEA

22 Julai 2019

Shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA, leo Jumatatu 22 julai 2019 limetangaza kwa masikitoko makubwa kifo cha aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Yukiya Amano.

Amano raia wa Japan na mwanadplomasia aliyekuwa na umri wa miaka 72 ameliongoza shirika la IAEA tangu mwaka 2009 na kabla ya kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo alifanya kazi katika utumishi wa umma wa kimataifa kwenye Umoja wa Mataifa katika vitengo mbalimbali .

Mwanadoplomasia huyo wa miaka mingi alikuwa chachu kubwa ya majadiliano kuhusu nyuklia ya Iran mwaka 2015 ambapo muafaka ulifikiwa baina ya Iran na Marekani uliojulikana kama mkakati wa pamoja wa hatua au JCPOA, ingawa mwaka jana Marekani iliamua kujiengua katika muafaka huo.

Mwendazake huyo pia alishiriki katika mikutano mbalimbali ya kutathimini mikataba kuhusu kupinga uzalishaji wa nyuklia katika miaka aliyohudumua IAEA.

Uongozi wa IAEA umesema kumpoteza Amano ni pigo kubwa kwani alikuwa mchapa kazi aliyeipenda kazi yake kwa moyo wote, pia umesema hivi karibuni aliandika barua ambayo angeiwasilisha kwa bodi ya magavana wa shirika hilo akitangaza uamuzi wake wa kutaka kujiuzulu na sehemu ya barua hiyo inasema “

“Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Shirika limeleta matokeo halisi ili kufikia lengo la Atomiki kwa ajili ya amani na maendeleo, kutokana na msaada wa nchi wanachama na kujitolea kwa wafanyakazi wa shirika hili. Ninajivunia sana mafanikio yetu, na ninawashukuru nchi wanachama na wafanyakazi wa shirika hili. "

Rambirambi zimekuwa zikitolewa na mashirika na watu mbalimbali kufuatia kifo hicho cha Bwana amano. Rais wa baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa kupitia ukurasa wake wa twoitter ameandika” nimesikitishwa sana na Habari za kifo cha Bwana Yukiya Amano mkurugenzi mkuu wa IAEA ambaye alifanyakazi bila kuchoka , kuchagiza dunia salama bila nyuklia. Wajibu wake asilani hautosahaulika, natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia yake na wanafanyakazi wote wa IAEA.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC Yuri Fedotov kupitia ukurasa wake wa Twitter ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Amano, marafiki na wafanyakazi wa AIAEA akisema “ilikuwa ni heshima kubwa kwangu kufanya naye kazi daiama atakumbukwa.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter