Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 50 baada ya walioenda mwezini kutua ardhini, UN bado inaunga mkono harakati

Picha hii mwanaanga Neil Armstrong akiwa mwezini (20 Julai 2019)
UN /NASA
Picha hii mwanaanga Neil Armstrong akiwa mwezini (20 Julai 2019)

Miaka 50 baada ya walioenda mwezini kutua ardhini, UN bado inaunga mkono harakati

Masuala ya UM

“Sisi wakazi wa dunia, ambao tunaweza kutatua matatizo ya sayari hii, tunaweza kutatua matatizo  yatokanayo na kuishi kwenye sayari hii,” ni kauli yake Neil Armstrong, binadamu wa kwanza kufika mwezini, kauli ambayo alitoa mara baada ya kutembelea Umoja wa Mataifa wiki tatu baada ya safari yao hiyo ya kipekee.

Wanaanga wa Marekani Neil Armstrong,  Edwin E. Aldrin, Jr. na Michael Collins ambao walisafiri na chombo Apollo 11 hadi mwezini walipotembelea Umoja wa Mataifa tarehe 13 Agosti 2019 baada ya safari yao.
UN /J. Grinde
Wanaanga wa Marekani Neil Armstrong, Edwin E. Aldrin, Jr. na Michael Collins ambao walisafiri na chombo Apollo 11 hadi mwezini walipotembelea Umoja wa Mataifa tarehe 13 Agosti 2019 baada ya safari yao.

Katika safari yake kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Armstrong, aliambana na wanaanga wenzake ambao walisafiri kwa chombo kiitwacho Apollo-11 hadi mwezini, ambao ni Edwin Aldrin na Michael Collins.

Leo hii, dunia ikiadhimisha robo karne tangu binadamu kwenda mwezini, Umoja wa Mataifa unakumbuka pia ziara ya wanaanga hao tarehe 13 Agosti mwaka 1969.

 “Hakuna mtu yeyote hapa ambaye hakushuhudia wanaanga hao wakitembea hatua za kipekee mwezini. Wakati huo, mamia kati yetu kupitia redio na televisheni tulishiriki katika tukio hili la kihistoria,” alisema Katibu Mkuu wa wakati huo U Thant.

“Chombo cha Apollo-11 kilifika salama mwezini na kurejea kwa mafanikio makubwa ardhini na kutudhihirishia kile ambacho binadamu anaweza kufanikisha kwa kutumia rasilimali zilizopo na teknolojia pindi binadamu hao wakishirikiana kwa maslahi ya binadamu wote,” alisema Bwana U.

Wakati wa ziara yao kwenye Umoja wa Mataifa, wanaanga hao walikabisha zawadi ambayo ni bapa la kumbukumbu linalofanana na lile waliloacha mwezini likiwa na maneno: "Hapa, binadamu kutoka sayari ya dunia walitua mwezini Julai 1969 baada ya kuzaliwa kristo. Tumefika kwa amani kwa ajili  ya binadamu wote.”

Kumbukumbu zingine ambazo zimehifadhiwa kwenye Umoja wa Mataifa kikihusiana na safari hiyo, ni sampuli mfano wa mwamba wa  mwezi.

Hii ilikuwa ni zawadi kutoka kwa Rais Richard Nixon, wa Marekani, zawadi ambayo ilikabidhiwa tarehe 20 mwezi Julai mwaka 1970 wakati jamii ya kimataifa ilipoadhimisha mwaka mmoja tangu safari ya Apollo-11 mwezini.

Wanaanga hao watatu Armstrong, Aldrin na Collins, walifika tena Umoja wa Mataifa na kushiriki kwenye hafla maalum ya kukabidhi jiwe hilo.

Pichani ni  wataalamu watatu, Armstrong , (wa pili kushoto), Aldrin, (wa tatu kulia) na Collins, (wa pili kulia) wanatembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa, na Katibu Mkuu U Thant (katikati) akiwa na jiwe kutoka mwezini na bendera (Julai 1970) .
Picha/Yutaka Nagata
Pichani ni wataalamu watatu, Armstrong , (wa pili kushoto), Aldrin, (wa tatu kulia) na Collins, (wa pili kulia) wanatembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa, na Katibu Mkuu U Thant (katikati) akiwa na jiwe kutoka mwezini na bendera (Julai 1970) .

Rais wa Baraza Kuu kushiriki maadhimisho ya miaka 50 tangu Apollo-11 kutua mwezini

Mapema jana Ijumaa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa alikuwa mgeni rasmi kwenye tukio maalum la maadhimisho ya miaka 50 ya chombo cha Apollo-11 kutua mwezini, tukio ambalo liliandaliwa na kampuni ya Google.

Katika tukio hilo, Bi. Espinosa aliungana na wanaanga wanawake kutoka shirika la anga za juu la Marekani, NASA, wajasiriamali, wataalamu wa tabianachi, wanaanga, vijana na wanachama wa chama cha masual ya anga za juu cha New York, NYSA.

Tukio hilo pia liliangazia jinsi ya kuchagiza ubunifu na ujasiriamali ambao unachochea zaidi wanawake kushiriki masuala ya anga za juu.

Bi. Espinosa amekuwa mchechemuzi wa kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu nyanja za sayansi, teknolojia, uhandishi na hesabu, STEM.

Duniani kote, wanawake ni chini ya asilimia 30 ya watafiti wote na ni chini ya theluthi moja tu ya wanafunzi wanawake ndio huchagua masomo ya STEM wanapojiunga na elimu ya juu.