WFP na Luxembourg zashirikiana kurahisisha mawasiliano kwenye majanga

18 Julai 2019

Manufaa ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi yameendelea kudhihirisha na hivi sasa ni katika sekta ya mawasiliaoni wakati wa majanga ambapo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP na serikali ya Luxembourg wamewezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa zaidi ya mawasiliano wakati wa majanga.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo huko Luxembourg imesema teknolojia hiyo imewezesha watoa huduma za misaada na waokoaji kuwasiliana na kubadilishana taarifa katika mazingira hatarishi na hivyo kuokoa maisha na kuhakikisha mahitaji ya jamii yanafikishwa haraka iwezekanavyo.

Ubia kati ya serikali hiyo ya Luxembourg na WFP pamoja na kikundi cha mawasiliano wakati wa dharura, ETC ulipatiwa chepuo zaidi na mafunzo yaliyotolewa hivi karibuni na taasisi ya Let’s Net ikileta washiriki kutoka mataifa 14 yakiwemo Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Yemen.

Familia ambazo ni manusura wa kimbunga Idai , zikihamishiwa kutoka makazi ya muda huko IFAPA mjini BEIRA kwenda kituo jirani na makazi yao ya awali wilayani Buzi nchini Msumbiji.
© UNHCR/Luiz Fernando Godinho
Familia ambazo ni manusura wa kimbunga Idai , zikihamishiwa kutoka makazi ya muda huko IFAPA mjini BEIRA kwenda kituo jirani na makazi yao ya awali wilayani Buzi nchini Msumbiji.

Akizungumzia ubia huo, Afisa mnadhimu mkuu wa WFP  Rehan Asad, amesema,  “ubia kati ya Luxembourg na WFP unaleta tofauti halisi kabisa pale maisha yanapokuwa hatarini. Tumeshuhudia baada ya vimbunga Idai na Kenneth nchini Msumbiji  ambapo wafanyakazi wa kibinadamu walipata mafunzo kupitia Let’s Ne walikuwa na mchango mkubwa katika kusambaza huduma za mawasiliano kule ambako zilihitajika zaidi.”

Washiriki wa mafunzo hayo walifundishwa jinsi ya kuandaa mawasiliano kwenye majanga na jinsi ya kufikisha taarifa hizo kwa wahusika ili maisha yaweze kuokolewa.

ETC ni mtandao wa kimataiwa wa mashirika ya kibinadamu, sekta binafsi na mashirika ya kiraia ambayo yanashirikiana kusambaza taarifa muhimu wakati wa majanga.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter