Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wako njia panda Syria, hali ya kibinadamu ni tete:UNICEF

Wakimbizi wakiwa kambi ya Al-Hol katika jimbo la Hasakeh kasakzini mashariki mwa Syria.
UNICEF/UN037295/Soulaiman
Wakimbizi wakiwa kambi ya Al-Hol katika jimbo la Hasakeh kasakzini mashariki mwa Syria.

Watoto wako njia panda Syria, hali ya kibinadamu ni tete:UNICEF

Amani na Usalama

Maelfu ya watoto wako njia panda nchini Syria wakiwemo wanaoshi kwenye kambi ya wakimbizi ya Al-Hol na sehemu zingine kutokana na manyanyaso, ukatili na hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea kutokana na vita.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo imesema takriban watu 70,000 wanaishi kwenye kambi ya Al-Hol Kaskazini mwa Syria na inakadiria kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu hao ni wanawake na watoto.

Karibu watoto 20,000 kambini hapo ni Wasyria na waliosalia 29,000 wanatoka katika nchi 62 tofauti wakiwemo 9,000 kutoka nchini Iraq na wengi wao wana umri wa chini ya miaka 12.

Kwa mujibu wa UNICEF wengi wa Watoto haw ani manusura wa vita kubwa na wameshuhudia unyama na ukatili wa hali ya juu. Shirika hilo la watoto linasema Watoto kwenye kambi ya Al-Hol wako katika hali mbaya sana ya kibinadamu hasa kwa kupitia ukatili au kushinikizwa kushiriki vita na kutekeleza vitendo vya kikatilikupindukia.

Hata hivyo shirika hilo linasema hwa ni sehemu tu ya idadi kubwa ya watoto wanaodaiwa kuhusishwa na vita vya silaha, waliokwama makambini, tumande, na kwenye vituo vya watoto yatima katika sehemu mbalimbali za Syria na hususan Kaskazini Mashariki.

Duru zinasema watoto wengi wanashikiliwa katika vituo mbalimbali na wengine wana miaka 12 tu na wanaendelea kuwa katika hatari kubwa wakati machafuko yakiendelea na kuongezeka katika baadhi ya sehemu Syria.

Watoto wakiwa katika hema wanalolitumia kama darasa katika kambi ya wakimbizi ya Junaina kaskazini mwa Idlib, Syria.
UNICEF/UN0248439/Watad
Watoto wakiwa katika hema wanalolitumia kama darasa katika kambi ya wakimbizi ya Junaina kaskazini mwa Idlib, Syria.

Katika jimbo la Idlib UNICEF inasema karibu watoto milioni 1 wamekwama kwa miezi kadhaa huku kukiwa na mapigano makali yanayoendelea.

Shirika hilo limeongeza kuwa licha ya kwamba machafuko yanapungua katika baadhi ya sehemu na wimbi la wanaokimbilia Al-Hol linapungua mahitaji ya kibinadamu bado ni changamoto kubwa ikiwemo fursa ya kupata maji salama na huduma za afya.

Hivi sasa UNICEF inatoa wito wa kuimarisha fursa za kibinadamu na ulinzi kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuwajumuisha katika jamii na kuwarejesha kwa usalama katika nchi zao.

Pia shirika hilo limezikumbusha pande zote kinzani katika mzozo wa Syria kwamba “hawa ni watoto na sio wahalifu, wana haki ya kulindwa ikiwa ni pamoja na kupata nyaraka za kisheria na kuunganishwa na familia zao.” Na imeziomba nchi zote wanachama zinazohusika kwa njia moja au nyingine na kinachoendelea Syria kuchukua hatua kwa kuzingatia maslahi ya watoto na kutimiza viwango vya sheria za kimataifa, na pia pande zote katika mzozo kuhakikisha fursa za kufikisha misaada ya kibinadamu zinapatikana