Ebola sasa ni dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi jumuiya ya kimataifa- WHO

17 Julai 2019

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limetangaza leo Jumatano kwamba ebola ni janga nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC na ni dharura ya afya ya umma inayotia  wasiwasi jumuiya ya kimataifa.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus katika tarifa yake  amesema “ni wakati wa dunia nzima kujifunza na kuimarisha juhudi zao maradufu. Ni lazima tufanye kazi kwa pamoja na DRC ili kutokomeza janga hilo na kujenga mifumo bora ya kiafya.”

Mkurugenzi mkuu huyo ameongeza kwamba, “kazi kubwa imefanywa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika mazingira magumu sana. Sisi sote, sio tu kutoka WHO lakini pia serikali, wadau na jamii tunahitaji kushirikiana kubeba mzigo.

Tangazo hilo la dharura ya afya ya umma limekuja kufuatia mkutano wa kamati ya kimataifa ya usimamizi wa afya. Kamati imetaja mabadiliko ya janga la ebola hivi majuzi nchini DRC katika mapendekezo yake ikiwemo kujumuisha kisa cha kwanza kilichothibitishwa Goma, mji wa watu takriban watu milioni mbili karibu na mpaka wa Rwanda na ambapo ni kituo cha mpaka wanakopita watu wengi kuingia nchi hiyo.

Kamati imeelezea kusikitishwa kwake na kukawia kwa ufadhili ambao unakwamisha juhudi za kukabiliana na mlipuko huku ikikumbusha kwamba ni muhimu kulinda vitega uchumi vya waathirka kwa kuweka mbinu za usafiri na mipaka wazi. Aidha wamesisitiza umuhimu wa kujizuia na hatua ambazo zitaathiri uchumi ikiwemo vikwazo dhidi ya usafiri na biashara ambazo huelekezwa kwa jamii zilizoathirika.

Tangu mlipuko wa ebola ulipotangazwa takriban mwaka mmoja uliyopita, umetajwa kama kiwango cha tatu cha dharura ikimaanisha iliyo mbaya zaidi na hivyo kusababisha WHO kufanya kazi kubwa zaidi.

Halikadhalika Umoja wa Mataifa upana wa dharura na kuimarsiha mifumo ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mlipuko.

Dkt. Tedros ameongezwa kwamba, “ni akina mama, wanaume na watoto na kwa mara nyingi familia nzima zinaathirika. Jamii na majanga binafsi yako moyoni, tangazo la leo la dharura ya afya ya umaa haipaswi kutumika kuwanyanyapaa na kuwaadhibu watu wale ambao wanahitaji msaada wetu kwa kiasi kikubwa.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter