Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunashikamana na AU kuhakikisha utawala wa kiraia unarejea Sudan: Haysom

Nicholas Haysom mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Sudan akihojiwa na UN
UNTV
Nicholas Haysom mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Sudan akihojiwa na UN

Tunashikamana na AU kuhakikisha utawala wa kiraia unarejea Sudan: Haysom

Amani na Usalama

Habari zilizotolewa leo na duru mbalimbali zinasema pande kinzani nchini Sudan zimetiasaini makubaliano ya kisiasa, na majadiliano zaidi yataendelea Ijumaa Julai 19 wiki hii katika masuala nyeti ambayo ni “kukubaliana kuhusu azimio la katiba ya mpito ambayo itaamua mfumo wa kushirikiana madaraka kati ya TMC na FFC, ikiwemo mfumo wa vyombo vya utawala na ni asilimia ngapi iende kwa kila upande katika baraza la Rais.”

Akizungumza awali na UN News mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mgogoro mpya wa saudan Nicholas Haysom amesema Umoja wa Mataifa unashikamana na Muungano wa afrika AU, katika kuhakikisha utawala wa kiraia unarejea nchini Sudan.

Bwana Haysom amesema Sudan imepitia madhila mengi na hivi sasa ipo katika kipindi muhimu cha mpito cha kuwahakikishia watu wake, ulimwengu na jumuiya ya kimataifa kwamba inataka amani, utulivu na mustakabali bora ambayo ndio matakwa ya wengi ikiwemo ukanda mzima

(SAUTI YA NICHOLAS HAYSOM )

“Endapo mambo yatakwenda vizuri kwa Sudan basi hali itakuwa shwari kwa eneo zima la Pembe ya Afrika, na endapo yatakwenda vibaya basi yatakuwa na athari kubwa kwa baadhi ya nchi ukizingatia kwamba tuna nchi kama Somalia kwa upande mmoja, tuna mgogoro Sinai kwa upande mwingine tuna Jamhuri ya Afrika ya Kati, tunayo Sudan Kusini inayojaribu kufufua mkataba wa amani , tuna Ethipia inayopitia majaribukwa hakika ni eneo ambalo liko katika hali tete. Na endapo tutaweza kutatua mgogoro wa Sudan , kusema ukweli faida zake zitakuwa nyingi katika kuleta utulivu wa eneo hilo kubwa”

Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya mji mkuu Khartoum Sudan Aprili 11, 2019
Ahmed Bahhar/Masarib
Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya mji mkuu Khartoum Sudan Aprili 11, 2019

Na je azma hiyo isipotimia?

(SAUTI YA NICHOLAS HAYSOM )

“Muungano wa Afrika AU, uliweka bayana masuala manne ya kutekeleza na kusema kwamba Sudan itasitishwa uanachama wa AU na mfumo wake endapo haitorejesha utawala kwa serikali ya kiraia. Au ilikuwa nguzo muhimu na nandhani Katibu Mkuu amelitambua hilo na ameniomba kuunga mkono jitihada za AU, ikimaanisha kwamba sio kuendesha tena mchakato tofauti wa Umoja wa Mataifa , lakini kuunga mkono AU na nafikiri hii ni katika kuanzisha msingi mpya wa ushirikiano.”

Ameongeza kuwa na kwa mantiki hiyo anaichagiza jumuiya ya kimataifa kuunga mkono msimamo wa AU. Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa bado unashikamana na watu wa Sudan

(SAUTI YA NICHOLAS HAYSOM)

“Haujawatelekeza watu wa Sudan na unaendelea kufikisha huduma muhimu na misaada ya kibinadamu kwa watu wa Sudan. Kwa mtazamo wangu tumemekuwa tukilenga msaada wetu ili kuhakikisha kwamba jumuiya ya kimataifa iko katika upande mmoja, inaunga mkono mkakati wa AU. Lakini kwas asa tuko katika kipindi cha kusaidia , watu wa sudan wanajiandaa kusimama kidete na serikali ya mpito, kuianzisha na kuisaidia ifanye kazi.”