Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo cha kaya ni muarobaini wa lishe duni duniani- FAO

Teknolojia ya nyuklia imeasaidia wakulima na familia zao nchini Zimbabwe
IAEA Video
Teknolojia ya nyuklia imeasaidia wakulima na familia zao nchini Zimbabwe

Kilimo cha kaya ni muarobaini wa lishe duni duniani- FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kaya zinazojihusisha na kilimo zinahitaji sera wezeshi za umma ili ziweze kuendana na kustawi katika mazingira ya sasa yanayobadilika kila uchao, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva.

Akizungumza mjini New York, Marekani wakati wa uzinduzi wa muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha kaya  kando mwa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu maendeleo endelevu, HLPF, Bwana da Silva amesema “tunahitaji kurekebisha mifumo yetu ya chakula na kuihusisha na shughuli za muongo wa kilimo cha kaya sambamba na muongo wa hatua za kuimarisha lishe.”

Amesema kuwa wakulima katika ngazi ya kaya ndio ambao wanazalisha vyakula vyenye afya na wanaweza kuokoa jamii dhidi ya utipwatipwa, “na tunawahitaji kwa ajili ya mlo wenye afya.”

FAO inasema kwa sasa mashamba ya kaya ni zaidi ya asilimia 90 ya mashamba yote duniani na yanazalisha asilimia 80 ya thamani yote ya vyakula duniani.

Akitambua kuwa ijapokuwa wakulima wa kaya wanatoka kona mbalimbali na hakuna mpango mmoja ambao unaweza kukidhi mahitaji yao yote, Bwana da Silva ametaja mambo makuu mawili ambayo yanaweza kusongesha muongo wa kilimo cha kaya.

Ametaja mambo hayo kuwa ni mosi; FAO na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD wameanzisha fuko la wahisani na kwamba tayari FAO imetenga fedha za kuanzia kusongesha mazungumzo na mawasiliano baina ya wakulima kuhusu sera za umma.

Wakulima huko São Tomé na Príncipe sasa wanaweza kumwagilia mashamba yao hata wakati wa msimu wa kiangazi na hivyo kuongeza uzalishaji.
UNDP/ São Tomé na Príncipe
Wakulima huko São Tomé na Príncipe sasa wanaweza kumwagilia mashamba yao hata wakati wa msimu wa kiangazi na hivyo kuongeza uzalishaji.

Pili, amesihi mataifa yasongeshe mipango yao ya utekelezaji ya kitaifa kwa kuzingatia mpango wa kimataifa wa utekelezaji wa FAO na IFAD ambao ulizinduliwa mwezi Mei mwaka huu akisema kuwa, “kwa njia hii FAO na IFAD zitaelewa vyema mahitaji na michakato ya kila nchi.”

Wakulima wa ngazi ya kaya ni wachochezi wa lishe bora

Katika hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu  huyo wa FAO ameonesha wasiwasi wake kuhusu ongezeko la viwango vya utapiamlo duniani akisema kuwa, “tunapaswa kushughulikia  haraka ongezeko la utipwatipwa na ukosefu wa madini muhimu mwilini. Hali hii inapata zaidi watu wanaokula zaidi vyakula visivyo na lishe bora.”

Amegusia ulaji wa vyakula vilivyosindikiwa akisema ni vichocheo vikubwa vya utipwatipwa akisema kuwa, “vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi vina kiwango kidogo cha lishe bora, na vina mafuta yasiyo na afya, sukari, chumvi na viambato vya kuongeza ladha na kwa bahati mbaya ni bei yake si ghali na upatikanaji wake ni wa rahisi na zaidi ya yote unaweza kuvitengeneza kwa urahisi hususan kwa wakazi maskini wa mijini."

Ni kwa mantiki hiyo, Bwan da Silva amesema wakulima wa ngazi ya kaya wanaweza kuwa na dhima muhimu katika kuongeza uzalishaji na ulaji wa vyakula bora na vyenye afya na hivyo kuboresha lishe ya watu.

Miongoni mwa wadau wa  uzinduzi huo wa muongo wa kilimo cha kaya ni IFAD, FAO pamoja na waandaaji Costa Rica na Ufaransa sambamba na La Via Campesina, jukwaa la vijiji duniani na chama cha wakulima duniani.