Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kingono umeendelea kuwa jinamizi kwa wanawake Sudan Kusini:UNMISS

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umefanya warsha maalum kwa ajili ya kusaidia wanawake ambao wamekabiliwa na ukatili wa kingono na kusihi jamii kuripoti visa hivyo ili wahalifu wawajibishwe
UNifeed Video
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umefanya warsha maalum kwa ajili ya kusaidia wanawake ambao wamekabiliwa na ukatili wa kingono na kusihi jamii kuripoti visa hivyo ili wahalifu wawajibishwe

Ukatili wa kingono umeendelea kuwa jinamizi kwa wanawake Sudan Kusini:UNMISS

Haki za binadamu

Jinamizi la ukatili wa kingono umewasakama wanawake nchini Sudani Kusini kwa miaka sita sasa tangu kuzuka kwa vita bvya wenyewe kwa wenyewe na unaendelea kuwatia hofu kila uchao, sasa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS umeamua kuwapa mafunzo ya kuwatia moyo na kuchukua hatua.

Katika kambi hii ya ulinzi wa raia inayohifadhi wakimbizi wa ndani mjini Juba ndiko warsha hiyo maalum inapofanyika ikiwa imewaleta pamoja wanawake waathirika wa ukatili wa kingono, lengo kuu ni kuhakikisha wanawapa ujasiri wa kuendelea na Maisha lakini pia kwa jamii kuichagiza kuchukua hatua za kuhakikisha wahusika wanafikishwa katika mkono wa sheria.

Kwa miaka sita sasa wengi wa wanawake hawa waathirika wanaishi kwa hofu kubwa wakiogopa hata kuondoka kambini hapa kwa fira za kutendwa ukatili tena kwani vita vinaendelea. Miongoni mwao ni mkimbizi wa ndani Martha Nyakuma Balkul

(SAUTI YA MARTHA NYAKUMA)

Kinachosababisha ukatili wa kingono ni migogoro na vita wakati wote, hivyo wale waliojihami kwa silaha walikuwa wakibaka watu kwa nguvu kwa sababu wana silaha. Namuomba Mungu awasaidie watu wa Sudan Kusini ili tuweze kurejea katika maisha yetu ya awaliya amani na utulivu nchini mwetu.”

Mkataba wa amani uliosainia mwezi Septemba mwaka jana umepunguza machafuko na wanawake wengi wanachagua kuondoka kambini na kurejea makwao hata hivyo wanaogopa kuzungumzia madhila yaliyowafika kwa sababu ya unyanyapaa na kutopata msaada kutoka kwenye jamii. Huma Khan ni afisa mshauri wa UNMISS kuhusu ulinzi wa wanawake kambini hapo

(SAUTI YA HUMA KHAN)

“ Wengi wa wanawake hawa walibakwa au ubakaji unaendelea wakati mwingine wanapotoka nje ya kambi, ni muhimu sana kwa jamii kuelewa kwamba wanawake hawa wanahitaji kupaza sauti zao, kusaka huduma na kufikisha suala hili kwenye mfumo wa sharia ili baadhi ya wahusika waweze kuwajibishwa.”

 UNMISS inaendesha warsha hii baada ya baraza la makanisa la Sudan kusini kutoa waraka ukisema ukatili wa kingono ni moja wa uhalifu mbaya zaidi kutekelezwa vitani.