Miaka 25 baada ya ICPD, huduma bora za afya ya uzazi kwa vijana bado ni ndoto- Banice

Wanawake katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakijadili kuhusu kuzuia maambukizi ya mgaonjwa ya zinaa.
© UNHCR/Brian Sokol
Wanawake katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakijadili kuhusu kuzuia maambukizi ya mgaonjwa ya zinaa.

Miaka 25 baada ya ICPD, huduma bora za afya ya uzazi kwa vijana bado ni ndoto- Banice

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa, HLPF, limeendelea likiangazia masuala kadhaa ikiwemo maadhimisho ya miaka 25 tangu kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa idadi ya watu na maendeleo, ICPD, huko mjini Cairo nchini Misri.

Mkutano huo umeleta pamoja washiriki kutoka nyanja mbalimbali wakiwemo viongozi waaandamizi wa Umoja wa Mataifa, Mawaziri na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na yale ya kiraia.

Akihutubia washiriki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa mkutano huo ulikuwa wa kipekee kwa kuwa ulifanikiwa kuonesha uhusiano kati ya idadi ya watu, haki za binadamu, ukuaji uchumi endelevu na maendeleo endelevu sambamba na kuweka masuala hayo katika mtazamo wa pamoja na si tofauti tofauti.

Guterres amesema kuwa, “mkutano wa Cairo ulisisitiza kwa uhakika kuwa kuendeleza haki za wanawake na wasichana ni msingi wa kuhakikisha ustawi wa kila mtu, familia na mataifa. Ulitambua usawa wa jinsia kama sharti la ujumuishi, maendeleo endelevu na kusisitiza kuwa afya ya uzazi ni haki ya msingi.”

Hata hivyo amesema bado wanawake na wasichana wengi kote duniani wanakabiliwa na changamoto kubwa juu ya afya, ustawi na haki zao za kibinadamu.

Kwa  mantiki hiyo Guterres amesema, “kukamilisha masuala yaliyosalia ambayo yalipitishwa na ICPD kutatuweka katika mwelekeo mzuri wa kufanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu na kuhakikisha amani, ustawi na utu kwa wote.”

Wasichana wakijifunza masuala ya kuvunja ungo na hedhi kwenye darasa la wasichana pekee lililo chini ya mradi wa Umoja wa Mataifa huko Bol nchini Chad.
UN/Eskinder Debebe
Wasichana wakijifunza masuala ya kuvunja ungo na hedhi kwenye darasa la wasichana pekee lililo chini ya mradi wa Umoja wa Mataifa huko Bol nchini Chad.

Baada ya hotuba ya Guterres, washiriki kadhaa walizunguzma na miongoni mwao ni Banice Mbuki Mburu, mwakilishi kutoka ushirika wa mashirika ya kiraia barani Afrika kuhusu idadi ya watu na maendeleo amesema kufanikisha malengo ya maendelevu, SDGs ni msingi wa kufanikisha mpango uliofikiwa Cairo miaka 25 iliyopita.

Mathalani amesema, “hatuwezi kuzungumzia elimu jumuishi na sawia na fursa za wote kusoma wakati wote wa maisha bila elimu ya kina kuhusu afya ya uzazi. Bila hiyo wasichana wetu wanakwamishwa na mimba za umri mdogo na magonjwa ya zinaa.”

Ameenda mbali akisema kuwa ukosefu wa huduma bora za afya ya uzazi bado ni changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi cha sasa na kwamba “hatuwezi kufanikisha lengo namba 8 na 10 la SDGs iwapo wasichana wetu wanakuwa mama na kuishia kufanya kazi isiyo na malipo.”

Bi Mburu amesema ingawa kuna furaha kubwa ya harakati za kutokomeza ukeketaji huko Ethiopia na Kenya bado kuna machungu yatokanayo na mbinyo wa fursa za watu kukusanyika na kujadili mambo yao katika maeneo mengi Afrika akisema, “hii inakwamisha makubaliano ya ICPD huko Cairo, miaka 25 iliyopita.”

Hivyo amesema kuelekea mkutano wa miaka 25 ya ICPD utakaofanyika nchini Kenya mwezi Novemba mwaka huu, anatoa wito kwa serikali, Umoja wa Mataifa, wahisani na kila mtu achukue hatua sasa kuwekeza kwenye elimu bora, afya, stadi za maisha na fursa za kifedha kwa vijana.

Mkutano wa kimataifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo ulifanyika kuanzia tarehe 5–13 Septemba mwaka 1994 mjini Cairo, Misri na kupitisha malengo makuu manne ambayo ni elimu kwa wote ifikapo mwaka 2015, kupunguza vifo vya watoto wachanga na watoto, kupunguza vifo vya wajawazito na kuhakikisha kuwa huduma za afya ya uzazi ikiwemo uzazi wa mpango zinapatikana kwa watu wote.