Miaka 25 baada ya Beijing kuna nuru lakini bado wanawake wanabaguliwa- Espinosa

15 Julai 2019

Hakuna taifa lolote duniani ambalo limefikia usawa kamilifu wa kijinsia nab ado wanawake wanaendelea kukabilia na ubaguzi kwenye kanda zote duniani, amesema hii leo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Espinosa wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika jijini New York, Marekani kuangazia usawa jinsia na fursa za uongozi wa wanawake katika dunia endelevu.

Katika hotuba yake hiyo, Bi. Espinosa ametaja ubaguzi uwe kwa misingi ya fikra potofu, hadi sheria za kibaguzi, kandamizi na ghasia.

Amesema “tumetoka mbali tangu kupitishwa kwa mpango wa utekelezaji wa Beijing miaka 25 iliyopita. Idadi ya wabunge wanawake imeongezeka maradufu na tuonavyo katika orodha ya wazungumzaji wetu hii leo, idadi ya wanawake walioshika hatamu si jambo la ajabu.”

Hata hivyo amesema kuwa bado wanawake wako nyuma katika suala malengo yote 17 ya maendeleo endelevu, SDGs akigusia suala la umiliki wa ardhi akitanabaisha kuwa, “ni asilimia 42 ya nchi zote duniani ambako wanawake wana haki sawa ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa wanaume ilhali ni asilimia 60 ya nchi ambazo zinawapatia wanawake fursa sawa na wanaume kwenye suala la huduma za kifedha.”

Photo UNAMA / Abbas Naderi
Uchaguzi wa wabunge nchini Afghanistan,20 Oktoba 2018.Bamyan.Wanawake wasimama katika mstari nje ya kituo kimoja wakijitarisha kupiga kura

Idadi zaidi ya wanawake viongozi kutanufaisha wengi- Bi. Mohammed

Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed amesema uwepo wa idadi kubwa zaidi ya wanawake kuanzia katika vyumba vya mikutano hadi mabungeni, kuanzia vyeo vya kijeshi hadi meza za kusaka amani, na hata ndani ya Umoja wa Mataifa, ina maana kwamba kuna idadi kubwa ya wanawake watoa maamuzi ambayo yatakuwa na manufaa kwa kila mtu.

Bi. Mohammed amesema kuwa, “iwapo tunataka kufanikisha SDGs, dunia  yetu inahitaji wanawake wengi zaidi hivi sasa. Na zaidi ya yote wanawake vijana zaidi kwenye uongozi, wakisimamia kidete usawa wa jinsia hali ambayo itaweka mazingira ya jamii zenye mnepo na hivyo kuwa na dunia yenye amani, ustawi na yenye afya.”

Katika mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake uliofanyika China mwezi Septemba mwaka 1995, nchi  189 zilikubaliana kile kilichoitwa Azimio la Beijing na mpango wa utekelezaji wenye kuzingatia usawa wa jinsia, azimio ambalo hadi leo hii linaonekana kuwa ni mwongozo thabiti na wenye kutia chagizo.

Tusipoteze wakati, hatuna muda- Bi. Mlambo-Ngcuka

Wakati wa mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya wanawake, UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema, “mwaka ujao tunapokuwa tunasherehekea miaka 25 tangu azimio la Beijing, maudhui yetu yatakuwa Kizazi cha usawa, kwa sababu, “tunasisitiza umuhimu wa ushiriki wa vizazi tofauti na dhima ya vijana katika kutusongesha mbele. Yote haya yanatupatia fursa ya kuongeza na kuendeleza ushiriki wa wanawake.”

Akizungumza huku akitazama saa yake, Bi. Mlambo-Ngcuka amesisitiza kuwa, “jamani hatuwezi kusubiri, muda umekwisha, kwa kweli muda umekwisha.”

Mkutano huo wa ngazi ya juu umeleta pamoja wanawake mashuhuri viongozi kutoka kona mbalimbali za dunia rais wa umoja wa mabunge duniani, Gabriela Cuevas Barron kutoka Mexico na Helen Clark ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter