Skip to main content

Vyakula vya watoto wachanga vina kiwango cha sukari kupita kiasi- WHO

Mama akimnyonyesha mwanae huko Ukraine wakati wa warsha mahsusi ya unyonyeshaji watoto wakati wa dharura, warsha iliyoandaliwa na UNICEF. (2015)
UNICEF/Zavalnyuk
Mama akimnyonyesha mwanae huko Ukraine wakati wa warsha mahsusi ya unyonyeshaji watoto wakati wa dharura, warsha iliyoandaliwa na UNICEF. (2015)

Vyakula vya watoto wachanga vina kiwango cha sukari kupita kiasi- WHO

Afya

Tafiti mpya mbili zilizofanywa na shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Ulaya zimebaini kuwa vyakula vinavyotangazwa kwa ajili ya watoto wenye umri wa chini ya miezi sita vinakiuka kanuni na vina kiwango cha juu cha sukari kupita kiasi.

Tafiti hizo zimefanywa kwa kukusanya takwimu kutoka vyakula au vinywaji 7955 vinavyouzwa kwa ajili ya watoto wachanga kutoka maduka 516 kwenye miji 4 ya Vienna, Austria; Sofia, Bulgaria; Budapest, Hungary; na Haifa, Israel kati ya mwezi November mwaka 2017 hadi mwezi Januari mwaka jana wa 2018.

Taarifa ya WHO kanda ya Ulaya iliyotolewa leo mjini Brussels, Ubelgiji, imesema katika miji yote hiyo minne, idadi kubwa ya bidhaa kati ya asilimia 28 hadi 60 ilitangazwa kuwa inafaa kwa ajili ya watoto wenye umri wa chini  ya miezi 6 kinyume na kanuni ya WHO inayokataza vyakula hivyo kutangazwa hivyo kwa kuwa watoto wenye  umri wa chini ya miezi 6 wanapaswa kunyonya maziwa ya mama pekee.

Halikadhalika katika miji mitatu, nusu ya bidhaa zilikuwa na zaidi ya asilimia 30 ya sukari na viambato vingine ambavyo vinachochea mtoto kupenda vyakula vyenye sukari.

Akizungumzia tafiti hizo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya, Dkt. Zsuzsanna Jakab amesema lishe bora tangu utotoni imesalia jambo la msingi katika kuchochea ukuaji wa mtoto na hali nzui ya baadaye kiafya.

Amesema kuepusha sukari kupita kiasi utotoni kunasaidia kuzuia uzito kupita kiasi, utipwatipwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo huchochewa na lishe duni na hivyo kwa kuzingatia vipimo sahihi itakuwa rahisi kufikia lengo namba 3 la malengo endelevu, SDG la kusongesha afya na ustawi kwa watu wote.

WHO inasema kuwa ijapokuwa vyakula kama matunda na mboga za majani kiasili vina sukari ambayo inafaa kwa watoto, bado vyakula vya rojo vinavyouzwa kibiashara vina kiwango cha juu cha sukari na kutia hofu kubwa.