Kila mtoto niliyekutana naye Beira amesema nyumba yao imebomoka-Guterres

12 Julai 2019

Mamia ya wanafunzi katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Msumbuji wa Beira wanaendelea kusoma katika madarasa yasiyo na paa hali aliyoishuhudia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anayeendelea na ziara nchini humo akizungumza na makundi mbalimbali ya waathirika wakiwemo watu wenye ulemavu.

Miongoni mwa mahali alipozuru leo Bwana Guterres ni shule ya June 25 ambako ameshuhudia uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Idai na kuacha asilimia kubwa ya madarasa ya shule hiyo bila paa. Akiwa katika madarasa mbalimbali ya shule hiyo Katibu Mkuu aliwauliza watoto hao walivyoathirika na kimbunga na kuna wakati wote waliinua mikono juu wakisema nyumba zao zimesambaratishwa kabisa na kimbunga hicho.

Guterres ameahidi kwamba shule hiyo itakarabatiwa na kuonekana vizuri tena na kwa watoto waliotaka kufahamu Umoja wa Mataifa ni kitu gani akawajibu”Ni sehemu ambapo nchi zote zinakutana kujaribu kutatua matatizo yanayoighubika dunia, wakati mwingine wanaweza na wakati mwingine wanashindwa.”

Akiwa bado shuleni hapo Katibu Mkuu alipata fursa ya kukutana na makundi ya watu wenye ulemavu ambao walinusurika katika kimbunga hicho. Watu wa makundi hayo wamesimulia ushuhuda wao wakiwemo mwenye Ualibino, mlemavu wa viungo, mtu aliyepooza, kiziwi na mama ambaye mtoto wake anaishi matatizo ya akili.

Akihitimisha ziara shuleni hapo Guterres amesema, “ni wajibu wetu kufanya kila liwezekanalo kusaidia hususani makundi ya watu wasiojiweza ambao wameathirika zaidi kutokana na zahma hii.

Kisha akaelekea kwenye kambi ya watu waliotawanywa ya Mutua inayohifadhi maelfu ya familia zilizoathirika. Akizungumza na waandishi wa habari kambini hapo amesema “ingawa sio tena kilele cha zahma hii iliyosababishwa navimbunga viwili vikubwa hapa nchini , lakini ni lazima kuainisha ukubwa wa tatizo na haja ya kupata msaada wa kimataifa kwa waathirika.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud