Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu ya kifo dhidi ya watu 30 sana’a inatutia hofu-OHCHR

Hukumu ya kifo.
UN Photo.
Hukumu ya kifo.

Hukumu ya kifo dhidi ya watu 30 sana’a inatutia hofu-OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu imesema imeshtushwa na kutiwa hofu kubwa na hukumu ya kifo waliyokatiwa watu 30 na mahakama ya mwanzo maalum kwa makossa ya jinai mjini Sana’a nchini Yemen.

Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu mjini Geneva Uswis Ravina Shamdasani akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema wanaume hao 30 ambao wengi wao ni wanazuoni, wanafunzi na wanasisa wanahusiana na chama cha Islah ambacho kimekuwa mkosoaji mkubwa wa Houthi na walisomewa hukumu yao ya kifo Jumanne wiki hii.

Shamdasani ameongeza kwamba “ofisi ya haki za binadamu imepokea taarifa za kuaminika zikipendekeza kwamba wengi wa watu hao waliohukumiwa walikuwa ni waathirika wa kuwekwa rumande kinyume cha sheria pamoja na utesaji na aina nyingine ya ukatili wakiwa rumande.”

Walikamatwa na maafisa wa vikosi vya jeshi na wajumbe wa kamati mashuhuri inazohusiana na utawala wa Houthi katika maeneo mbalimbali mwaka 2016, na Aprili mwaka 2017 walifunguliwa mashitaka wakidaiwa kushiriki na kuunda kundi lenye silaha kwa lengo la kuendesha vitendo vya kihalifu dhidi ya wafanyakazi wa vikosi vya ulinzi na usalama na kamati mashuhuri za Houthi, uhalifu kama mashambulizi ya mabomu, na mauaji mjini Sana’a, kutoa msaada wa kijasusi kwa wahalifu na kuvuruga amani na usalama wa Yemen.

Ofisi ya haki za binadamu inasema inaelewa kwamba hukumu hiyo na vifungo vyao vitakatiwa rufaa hivyo imetoa wito kwa mahakama ya rufaa kutilia maanani madai ya utesaji na unyanyasaji mwingine na hata ukiukwaji wa kuwa na kesi ya haki na mchakato mzima dhidi ya washitakiwa. “makossa yote yaliyotokana na mrengo wa kiasa yanapaswa kufutwa na viwango vya kimataifa vya kuendesha kesi kwa haki vifuatwe. Kwani Umoja wa Mataifa unapinga matumizi ya hukumu ya kifo katika mazingira yoyote yale.”