Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa kuchukua hatua ni sasa wanawake na wasichana hawawezi kusubiri haki zao:UN

Manusura wa Fistula wakipewa huduma ya afya nchni Tanzania
© UNFPA Tanzania/Bright Warren
Manusura wa Fistula wakipewa huduma ya afya nchni Tanzania

Wakati wa kuchukua hatua ni sasa wanawake na wasichana hawawezi kusubiri haki zao:UN

Afya

Wakati idadi ya watu duniani ikikadiriwa kuongezeka na kufikia bilioni 9 mwaka 2050 Umoja wa Mataifa imezitaka nchi kuzingatia uwiano kati ya ongezeko la idadi ya watu na maendeleo

Katika ujumbe wake kuhusu siku ya idadi ya watu duniani hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030 ni kioo cha mustakabali bora kwa wote na sayari duniaa na hilo linaenda sambamba na mwenendo wa mazingira yetu ikiwemo ongezeko la idadi ya watu duniani, uzee, uhamiaji na ukuaji wa miji.

Amesema ili kufanikisha azma ya mustakbali bora kwa wote ni muhimu kutilia maanani uwiano baina ya watu waliopo na maendeleo kwani “wakati kwa ujumla idadi ya watu ikiendelea kuongezeka ukuaji huo hauko sawia. Kwan chi nyingi zenye maendeleo duni changamoto za maendeleo endelevu zinaghubikwa na ongezeko la idadi ya watu na pia mabadiliko ya tabia nchi huku kwengine wakikabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya wazee na kutokuwepo na hifadhi ya jamii.

Guterres amesema “wakati tukikabiliana na mwenendo wa idadi ya watu tunapaswa pia kutambua uhusiano uliopo baina ya ifdadi ya watu, maendeleo na mustakabali wa watu binafsi” amesema mkutano wa Cairo Misri wa mwaka 1994 (ICPD) uliweka bayana kuhusu hili na pia kutambua kwamba “kuchagiza uswwa wa kijinsia ni kitu sahihi kufanya na pia ni haki ya binadamu na moja ya njia mujarabu za zinazoaminika kuelekea utimizaji wa malengo ya maendeleo na kuboresha maisha ya watu wote.”

Kaulimbiu ya siku ya idadi ya watu mwaka huu ni “maisha yake, chaguo lake , mustakabali wetu” lakini Guterres amasema pamoja na hatua zilizopigwa katika kumkomboa mwanamke kama kupunguza vifo vya watoto wachanga , kina mama wakati wa kujifungua , na mimba zisizotakikana bado kuna changamoto lukuki na duniani kote tunashuhudia haki za wanawake zikirudishwa nyuma ikiwemo haki za huduma muhimu za afa na masuala yanayohusiana na ujauzito sababu ambayo inaongoza kwa vifo vya wasichana wa kati ya miaka 15 hadi 19, pia ukatili wa kijinsia  ambao miziz yake ni kutokuwepo usawa unaendelea kuathiri maisha ya mamilioni ya wanawake.

Akisisitiza hilo mkurugenzi mtendaji wa shirika la idadi ya watu duniani Dkt. Natalia Kanem amesema wanawake wana haki ya kufanya maamuzi kuhusu endapo, lini , na nani na kwa jinsi gani wapate ujauzito . Hata hivyo amesema licha ya hatua zilizopigwa bado safari ni ndefu ya kutimiza lengo la mkutano huo wa Cairo na wanawake wengi wanaachwa nyuma bila kuwa na uwezo wa kufurahia haki zao.

 ”wakati wa kuchukua hatua ni sasa, na tena haraka ili kuhakikisha kwamba kila mwanamke na msichana anaweza kufurahia haki zake.kukiwa na wigo mpana wa chaguo la njia za uzazi wa mpango wanawake wanaweza kushamiri kama wadau wakubwa wa maendeleo endelevu.Hakuna muda wa kupoteza mustakabali wetu unategemea hilo” Hivyo katika siku hii Dkt Kanem amesema ”Natoa wito kwetu sote, serikali, asasi za kiraia, jamii na watu kutoka kila sekta na aina ya maisha , kuwa na msimamo na majasiri kuwatendea haki wanawake na wasichana kote duniani ili kukamilisha safari tulioianza Cairo  kwani wanawake na wasichana hawawezi kusubiri tena.”