Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matibabu yanahitajika haraka kwa waliowekwa kizuizini nchini Iran-Wataalamu wa UN

Bendera(katikati) ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.
UN Photo/Loey Felipe
Bendera(katikati) ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

Matibabu yanahitajika haraka kwa waliowekwa kizuizini nchini Iran-Wataalamu wa UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, hii leo mjini Geneva Uswisi wameeleza wasiwasi wao kuwa pamoja na wito wa mara kwa mara, Iran inaendelea kuwanyima huduma ya afya watu wanaoshikiliwa kifungoni nchini humo.

Wataalamu hao wamenukuliwa wakisema, “kwa miezi kadhaa tumekuwa tukiwasiliana na serikali ya Iran kuhusu wasiwasi wetu wa hali ya afya ya wafungwa. Pamoja na serikali kutuhakikishia, tunasikitishwa bado kupokea ripoti za kunyimwa kwa matibabu ikiwemo hali inayotishia maisha. Matukio hiyo haya siyo tena tukio moja moja bali mfululizo wa matukio.”

Hali mbaya ya mwanaharakati wa haki za binadamu Arash Sadeghi ambaye imeripotiwa kuwa amegundulika kuwa na saratani nadra ambayo inashambulia mifupa, inatia wasiwasi. Sadeghi alihukumiwa miaka 15 jela na mahakama ya mapinduzi mnamo mwezo Agosti mwaka 2015 kwa tuhuma za “kukutana na kushiriki katika propaganda dhidi ya taifa”. Wataalamu wamesema harakati zake za kupigania haki za binadamu zilihusisha maandishi yake katika mitandao ya kijamii na pia kuwasiliana na wanahabari na wapigania haki za binadamu wengine duniani kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Iran.

Mamlaka za magereza katika gereza la Raja’i Shahr wameripotiwa kukataa kumpa matibabu mfungwa huyo na hali yake ya kiafya inazidi kudhoofika baada ya kurejeshwa gerezani kinyume na ushauri wa madaktari na hasa baada ya kufanyiwa upasuaji mwaka 2018.

Wasiwasi mkubwa pia umeelezwa kumuhusu Ahmadreza Djalali na Kamran Ghaderi. Djalali ni mtu mwenye uraia pacha wa Sweden na Iran, daktari na mtafiti katika taasisi ya tiba ya Karolinska mjini Stockholm. Alishitakiwa na kuhukumiwa kifo kwa madai ya kuipeleleza Iran. Amekuwa akishikiliwa katika gerza la Evin na ananyimwa nafasi ya kupata matibabu japokuwa vipimo vinaonesha anaweza kuwa na saratani.

Ghaderi naye mwenye uraia pacha wa Austria na Iran, pia mfanyabiashara alihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa madai ya kufanya ujasusi. Naye pia yuko katika gereza la Evin na amenyimwa nafasi ya kupata matibabu pamoja na kuwa na uvimbe wa saratani katika mguu wake.

Pia wataalamu wa haki za binadamu wameeleza uwepo wa wanawake wawili Nazanin Zaghari-Ratcliffe na Narges Mohammadi ambao hali yao ya afya ilielezwa tangu mwezi Januari mwaka 2019 lakini wameendelea kunyimwa matibabu.