Dunia haijafanya vya kutosha kushughulikia umaskini na mazingira

9 Julai 2019

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, malengo yaliyowekwa na viongozi wa dunia mwaka 2015 kushughulikia umaskini na mazingira hayajatekelezwa ipaswavyo.

 

Katika ripoti yake ya hivi karibuni [insert link] kuhusu hatua zilizopigwa kuelekea kufikiwa kwa malengo 17 ya maendeleo endelevu SDGs, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antono Guterres anasema kuwa ingawa hatua zimechukuliwa na serikali mbalimbali kote duniani, lakini watu na nchi zilizoko hatarini wanaendelea kuteseka zaidi.

Malengo 17 ya SDGs yanazitaka nchi kuhamasisha juhudi za kumaliza kila aina ya umaskini, kupambana na kukosekana kwa usawa na mabadiliko ya tabia nchi.

Ripoti hiyo inafuatilia maendeleo katika malengo 17 kwa nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa na kwa kiasi kikubwa inachukua mtazamo wa kimataifa, hata hivyo wakati mwenendo kuhusu SDG ni wa kawaida katika kanda zote, kuna tofauti kubwa za kikanda. Hapa kuna mambo sita ambayo inabidi kuyafahamu kuhusu hatua zilizofikiwa kwa baadhi ya malengo muhimu ya SDGs .

UNICEF/Uddin
Familia iliyoachwa bila makazi baada ya kimbunga Aila ikiwa inasubiri msaada huko Koira, Bangladesh.

Mabadiliko ya tabianchi

Ikielezwa na Bwana Guterres kwamba mwaka uliopita yaani 2018 kama tishio kwa uwepo wa binadamu, hatua ya kuyafikia malengo ya kupunguza mabadiliko ya tabia nchi ni mbaya. Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa hewa chafuzi, mabadiliko ya tabianchi yanayotokea kwa kasi kubwa kuliko iliyotarajiwa na madhara yake yanaonekana wazi kote duniani.

Lengo, la makubaliano ya viongozi wa dunia, ni kuhakikisha ongezeko la joto linabakia chini ya  2°C na ikiwezekana kufikia 1.5°C juu ya joto la kabla ya mapinduzi ya viwanda. Wastani wa joto la dunia tayari umefikia 1°C juu ya joto la kabla ya viwanda lakini ikiwa hakuna kubwa litakalofanyika, joto litaongezeka na linaweza kuzidi 3°C kufikia mwishoni mwa karne hii.

Ingawa kuna hatua nzuri kwa kuangalia nchi mojamoja zinazoendeleza mipango ya hali ya hewa na ongezeko la kiasi cha fedha kilichopatikana ili kufadhili shughuli hizo, Bw Guterres anasema "mipango ya kipaumbele zaidi na hatua za haraka zinahitajika" kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

OCHA/Giles
Familia iliyopoteza makazi ikiwa imejiegesha kwenye Hema nchini Yemen

Umasikini uliokithiri

Umaskini uliokithiri, ambao Umoja wa Mataifa unautafsiri kama hali ya kukosa kupata mahitaji ya msingi ya binadamu, umeendelea kupungua, lakini upunguaji umedorora kwa kiwango ambacho dunia haiko katika kasi ya kutosha kufikia lengo la kuwa chini ya asilimia 3 ya watu wanaoishi katika umasikini uliokithiri kufikia mwaka 2030. Inakadiriwa kuwa hivi sasa kiwango kiko katika asilimia 6 ambayo ni takribani watu milioni 420, hali ambayo ni ya kusikitisha, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Migogoro na majanga nayo yameonekana kuchangia. Katika ukanda wa nchi za kiarabu, umaskini uliokithiri, hapo awali ulikuwa chini ya asilimi 3 lakini migogoro nchini Syria na Yemen vimeongeza kiwango cha umaskini katika eneo hilo na kuwaacha wengi wakiwa na njaa na kukosa makazi.

Kihistoria kuna sababu za kuwa na matumaini. Kiujumla idadi ya watu duniani kote wanaoishi katika umaskini uliokithiri kwa mwaka 2015 ni asilimia 10 chini kutoka katika asilimia 16 ya mwaka 2010 na asilimia 36 kwa mwaka 1990.

OCHA/Meridith Kohut
Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo katika kliniki ya Madaktari wasiokuwa na mipaka katika kambi ya Dadaab, Kenya.

Njaa

Njaa imeongezeka tena duniani, kwa makadirio ya watu milioni 821 walio katika hali ya utapiamlo kwa mwaka 2017 imeenda juu kutoka 784 katika mwaka 2015. Kwa hivyo mtu mmoja kati ya watu tisa hawapati chakula cha kutosha.

Afrika inabaki kuwa bara ambalo lina kiwango kikubwa cha utapiamlo ukiathiri moja ya tano ya idadi ya watu wote wa Afrika ambao ni zaidi ya watu milioni 256. Uwekezaji wa jamii katika kilimo unapungua kote duniani, hali ambayo inatakiwa kuangaliwa kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. “Wazalishaji wa chakula kwa kiwango cha chini na wakulima wa kifamilia wanahitaji usaidizi mkubwa na uwekezaji katika miundombinu na teknolojia kwa ajili ya kilimo endelevu vinahitajika haraka.”

Nchi zinazoendelea zimeathirika zaidi na uhaba huu wa uwekezaji. Mgawanyo wa uzalishaji wa chakula katilka nchi za Afrika, Asia na Amerika ya kusini uko katika asilimia 40 hadi 85 ikilinganishwa chini ya asilimia 10 Ulaya.

UNICEF/Frank Dejongh
wanawake katika zahanati moja kwenye kijiji cha Hassian, kaskazini mashariki mwa Côte d'Ivoire wakisubiri watoto wao kupewa chanjo dhidi ya TB.

Afya

Hatua kubwa imepigwa katika kuboresha afya ya mamilioni ya watu, kuongeza viwango vya umri wa kuishi, kupunguza vifo vya wakati wa kujifungua na vya watoto wachanga pia kupambana na mgaonjwa hatari ya kuambukiza. Pamoja na mafanikio hayo, inakadiriwa kuwa wanawake 303,000 kote duniani walikufa kutokana na matatizo ya ujauzito na wakati wa kujifungua mnamo mwaka 2015, wengi wao wakiwa katika eneo la kusini mwa janngwa la Sahara.

Maendeleo yanazorota au hayatokei kwa kasi ya kutoka katika kushughulikia magonjwa makubwa kama vile Malaria na kifua kikuu japokuwa takribani nusu ya idadi ya watu wote duniani yaani watu bilioni 3.5 hawana uhakika wa huduma bora za afya.

Bwana Guterres anasema, “juhudi kubwa zinahitajika kufikia huduma ya afya kwa wote, ufadhili endelevu kwa ajili ya afya na kushughulikia mzigo unaokua wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonwa ya akili.”

Usawa wa kijinsia

Unyanyasaji wa kijinsia unaendelea. Duniani kote takribani asilimia tano ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa unyanyasaji wa kimwili au kingono na wapenzi wao katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Kiwango cha matukio hayo ni kikubwa katika nchi 47 maskini zaidi duniani, ambazo umoja wa Mataifa unaziita LDCs.

Ingawa baadhi ya dalili za usawa wa kijinsia zinaendelea, kama vile kupungua kwa ukeketaji na ndoa za utotoni, idadi ya jumla bado ni ya juu. Aidha masuala kama ubaguzi wa kisheria, mila za kijamii, maamuzi na masuala ya uzazi pamoja na ushiriki mdogo wa kisiasa vinakwaza juhudi za kufikia malengo.

Katabu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, “hakuna namna yoyote tunayoweza kuyafikia malengo 17 ya maendeleo endelevu bila kuufikia usawa wa usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana.”

World Bank/Enrico Fabian
Wafanyakazi wakiwa katika kituo cha kuendeleleza stadi za vijana mjini Delhi, India.

Kazi na Ajira

Wataalamu wanakubali kuwa ukuaji wa uchumi ambao unajumuisha nyanja zote za jamii na ambao ni endelevu, unaweza kusongesha na kuzalisha namna ya kutekeleza SDGs. Duniani, uzalishaji wa kazi unmeongezeka na kukosekana kwa ajira kumerudi nyuma kwa viango ambavyo vilionekana kabla kabla ya mdororo wa uchumi wa mwaka 2008, ingawa uchumi wa dunia unakuwa kwa kasi ndogo. Na vijana wadogo wako katika uwezekano wa kukosa ajira mara tatu kuliko watu wazima.

Bwana Guterres anasema “maendeleo zaidi yanahitajika kuongeza fursa za ajira hususani kwa vijana wadogo, kupunguza ajira zisizo rasmi na kupunguza pengo la malipo kati ya jinsia na kukuza mazingira salama ya kazi ili kutengeneza kazi bora kwa wote.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud