Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC sasa marufuku kuoa msichana wa chini ya miaka 18

Muathirika wa ukatili wa kingono mjini Goma DRC.
Picha ya UN/Marie Frechon (Maktaba)
Muathirika wa ukatili wa kingono mjini Goma DRC.

DRC sasa marufuku kuoa msichana wa chini ya miaka 18

Haki za binadamu

Mkutano  wa Kamati ya watalaam wa Baraza la Haki za Binadamu kuhusu ukomezaji wa mifumo yote ya kibaguzi dhidi ya wanawake CEDAW, unaendelea jijini Geneva Uswisi ambapo viongozi kutoka nchi mbalimbali wanajadili mikakati ya kutokomeza mifumo kandamizi kwa wanawake duniani kote. Leo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC imeelezea jinsi wanawake walivyopiga hatua.

Akizungumza katika mkutano huo hi leo, Bi Marie- Ange Mushobekwa ambaye ni waziri wa  haki za binadamu wa  DRC amesema ili kufikia azma ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake nchini yake imepiga hatua kwanza katika kutoa fursa za uongozi kwa wanawake katika ngazi ya watunga sheria yaani kwenye Bunge la taifa hilo na pia katika Mahakama.

 

(Sauti ya Marie- Ange Mushobekwa)

Ni ushindi mkubwa na ni jambo la kujivunia kwa nchini ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na watu wake, hasa kwetu wanawake kutoka Congo. Japo wanawake hawana uwezo wa kuchukua dola kwa nguvu ila kwa sasa wanawake wanafursa ya kuingia Bungeni  na pia kushika nafasi ya juu katika Mahakama kuu kwa njia ya kura. Hii ni kutokana mfumo wa kidemokrasia unaondelea hivi sasa katika nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara.

Na vipi kuhusu sheria zinazotetea haki za wanawake nchini humo? Bi Mushobekwa amesema.

(Sauti ya Marie- Ange Mushobekwa)

Kati ya hatua tulizopiga   hivi karibuni ni pamoja na mabadiliko ya kifungu cha sheria ya familia ambapo awali umri wa  msichana kuolewa ulikuwa ni miaka 14. Na baada ya madadiliko sasa hivi ni miaka 18. Hii ina maana kwamba hakuna kiongozi yoyote serikalini anayeweza kufungisha ndoa kwa mtoto.

Jitihada za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, ni moja katika hatua muhimu ya kufikia usawa wa kijinsia kama ilivyo katika ajenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa  au SDGs itakayofikia ukomo mwaka  2030.